KONGAMANO LA UPATIKANAJI WA FEDHA ZA NDANI ZA MAENDELEO LAFANYIKA JIJINI ARUSHA

CDF 1
Mratibu Mkazi Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) na Mwakilishili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez ambaye alikua mgeni rasmi katika Kongamano la upatikanaji wa fedha za ndani za maendeleo akitoa hotuba yake kwa washiriki kutoka Halmashauri za wilaya nchini lililofanyika jijini Arusha.
CDF 2
Mkuu wa Mfuko wa Umoja wa mataifa wa Ukuzaji Mitaji (UNCDF) nchini na Meneja wa LFI duniani, Peter Malika akizungumza wakati Kongamano hilo.
CDF 4
Mkurugenzi wa Huduma(Tamisemi), Denis Bandisa akizungumza wakati Kongamano ambalo pamoja na mambo mengine alizitaka halmashauri nchini kubuni vyanzo vya ndani vya mapato badala ya kutegemea wafadhili.
CDF 5
Washiriki kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi wakifatilia kwa makini mada katika Kongamano hilo.
CDF 6
Washiriki kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi wakiwa katika picha ya pamoja, Kongamano hilo limefanyika katika hoteli ya Mount Meru jijini Arusha.
Na Mwandishi wetu, Arusha
MFUKO wa Umoja wa Mataifa wa Ukuzaji Mitaji (UNCDF) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), umeitisha kongamano la siku mbili la upatikanaji wa fedha za ndani kwa maendeleo.
Kongamano hilo linahusisha wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa nchini Tanzania na linashirikisha watu 110.
Pamoja na wakurugenzi hao, wapo na wawakilishi kutoka Serikali Kuu na wawakilishi walioteuliwa kutoka serikali za mitaa za Uganda, Senegal na Benin.
Kwa mujibu wa taarifa ya UNCDF, nia ya kongamano hilo ni kuonesha mafanikio ya mfumo wa ukusanyaji wa fedha za ndani kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi ya kibiashara katika nchi za Tanzania na Uganda.
Taarifa hiyo imesema kwamba baada ya kujifunza mafanikio hayo washiriki watajadiliana na kujipanga kwa ajili ya utekelezaji wa mfumo huo katika nchi zao wanaokotoka ili kupiga hatua mbele katika uendelezaji wa miradi bila kutegemea fedha za nje.
Akizungumza wakati wa ufunguzi Katibu Mkuu Tamisemi, Jumanne Sagini alisifu kazi inayofanywa na programu ya uwezeshaji wa fedha za ndani kwa maendeleo ( Local Finance Initiative- LFI) chini ya sekretarieti ya UNCDF kwa ubunifu wake unaowezesha kupatikana kwa mitaji ya kuwekeza katika miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na serikali za mitaa.
Aidha alielezea dhamira ya serikali ya kutumia mfumo huo ulioasisiwa na UNCDF kwa kuufanya uwe wa kitaasisi zaidi ili kuweza kusaidia kutekeleza mipango ya maendeleo na uwekezaji ya serikali za mitaa.
Akizungumzia umuhimu wa kongamano hilo, Mgeni rasmi, Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Alvaro Rodriguez, aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kufuata mfumo wa utafutaji wa fedha za ndani kwa ajili ya kukuza uwekezaji katika miundombinu ya kibiashara inayoleta mabadiliko kwa umma.
Rodriguez alisema katika hotuba yake kwamba kwa kuwezesha mfumo wa UNCDF LFI kwenye serikali za mitaa ndio jibu la uhakika la uwekezaji wenye mafanikio endelevu kwa taifa zima.
Aidha alisema mpango huo wa LFI ambao umekuwepo nchini kwa miaka mitatu na kuwezesha kuleta mabadiliko katika jamii, unafaa kumilikiwa na jamii ili kuwezesha mafanikio ya juu katika uwekezaji.
Mratibu huyo alisema kwamba Umoja wa Mataifa kupitia UNCDF utaendelea kufanyakazi na serikali ya Tanzania,kwa kuwa wanaamini kwamba vita dhidi ya umaskini itafanikiwa kwa kuhamisha mitaji na kuipeleka katika ngazi za chini kwa maendeleo ya wananchi.
Kongamano hilo ambalo ni mwendelezo wa uwezeshaji na kubadilishana uzoefu na elimu kwa lengo la kuwezesha miradi ya umma na binafsi inayochagiza maendeleo kujengwa; katika siku ya kwanza ya kongamano hilo washiriki wataoneshwa miradi iliyotekelezwa manispaa ya Busia Uganda na Kibaha nchini Tanzania.
Manispaa ya Busia imejenga kituo cha malori, ushuru wa forodha na maeneo ya kufanyia biashara, wakati Kibaha wamejenga kituo cha kisasa cha mabasi na soko.
Timu ya wataalamu wa UNCDF watawafundisha washiriki kwa siku 2 kuhusu miradi ya maendeleo, awamu za malipo ya fedha na mikakati ya kupata fedha na malipo na mbinu za kupunguza hatari za kibiashara.
Akisisitiza umuhimu wa kongamano hilo Mkuu wa UNCDF nchini na Meneja wa LFI duniani Peter Malika alisema kwamba kongamano hilo linatoa nafasi kwa watumishi wa serikali za mitaa na wengine kujifunza namna mpya ya kupata mitaji kwa kutumia vyanzo vya nyumbani ili kufadhili miradi ya miundombinu ya kiuchumi inayohitajika kwa ajili ya kutoa fursa za ujasiriamali , biashara, uwezeshaji, ajira, kuboresha maisha ya watu, ukusanyaji kodi na utoaji huduma.
Kongamano hilo la siku 2 ni miongoni mwa juhudi kadha za UNCDF za kuwezesha serikali za mitaa kufikia maendeleo endelevu na kuleta athari chanya kwa jamii ili kuondoa umaskini.
Share on Google Plus

About Jestina George

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment