SHIRIKA LA MADINI LA TAIFA (STAMICO), LAELEZEA MAFANIKIO YA MIRADI YAKE MBALIMBALI

 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),  Zena Kongoi.
Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa STAMICO, Deusdedith Magala, akizungumza na wanahabari.
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),  Zena Kongoi (kulia), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana, kwenye maonyesho ya wiki ya utumishi wa umma yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja kuhusu mafanikio yaliyofikiwa na shirika hilo katika miradi mbalimbali. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa Stamico, Deusdedith Magala.
Madini mbali mbali yaliyopo katika banda la shirika hilo.
Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa STAMICO, Deusdedith Magala (katikati), akizungumza na wanahabari kuhusu mikakati ya maendeleo ya miradi mbalimbali inayofanywa na Stamico.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),  Zena Kongoi (wa pili kushoto), akiwa na viongozi wenzake. Kutoka kulia ni Meneja Masoko na Uhusiano kwa Umma, Koleta Njelekela, Mhandisi Migodi Mwandamizi, Ibrahim Dauda, Mjiofizikia, Denis Silas na Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa STAMICO, Deusdedith Magala.


Na Dotto Mwaibale

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limeanzisha miradi mbalimbali ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini ili kuwaendeleza kutoka katika uchimbaji duni usiozingatia kanuni.

Kuanzishwa kwa miradi hiyo kunatokana na wachimbaji hao kutokuwa na maeneo maalum ambapo  itawasaidia wachimbaji hao kufikia kiwango cha uchimbaji wa kati chenye tija, ambapo ni muendelezo wa mradi wa kuratibu na kuwaendeleza.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo maonesho ya wiki ya utumishi wa umma yanafanyika jijini Dar es Salaam leo mchana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Zena Kongoi alisema shirika hilo limepata mafanikio mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2014 hadi mwaka huu wa 2015.

Alisema kupitia mradi huo, shirika limeweza kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini ya bati wa Wilaya ya  Kyerwa kupata soko la madini hayo, jambo ambalo limesaidia kupunguza utoroshaji wake kwenda nchi jirani na kuiongezea serikali mapato.

"Tumewawezesha kwa kuwapa ushauri wa kitaalamu na kiufundi kwa wachimbaji wadogo mbalimbali. Lakini pia tunaelekea kukamilisha mchakato wa mfumo mtandao wa uchimbaji mdogo utakaowawezesha kupata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu masoko, bei n aina bora za vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji," alisema.

Kongowi alisema kwenye mradi wa dhahabu unaosimamiwa na kampuni tanzu ya Stamigold Biharamulo Gold Mine, mgodi huo umeweza kuingiza Dola za Marekani milioni 14.2 katika kipindi cha Agosti, mwaka jana na Mei, mwaka huu.

Aliongeza kuwa mgodi huo pia umeanza kulipia ushuru wa huduma wa asilimia 0.3 kwa halmashauri ya Biharamulo na kuchangia pato la taifa kwa kurejesha mrahaba wa asilimia 4, ambapo wanatarajia kupata Sh. milioni 609 kama ada ya usimamizi wa mgodi huo.

Mbali na mafanikio hayo alisema zipo baadhi ya changamoto ambazo wanaendelea kuzishughulikia ambapo miongoni mwake ni upungufu wa mtaji kutokana na kuwa shirika hilo kwa sasa linafufua upya  miradi yake mingi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu, Deusdedith Magala alisema, kulingana na kauli mbiu ya mwaka huu ya maonesho hayo, shirika hilo linahakikisha linawasaidia akinamama kwa kuwatengezea mazingira mazuri ya kufanya kazi ndani ya shirika hilo.

Aliongeza kutokana na shirika hilo kuanza kazi upya katika kipindi cha mwaka jana walilazimika kuajiri wafanyakazi  wapya 87 ambapo wanawake ni 25 na wanaume 62 lengo likiwa ni kuwezesha shirika hilo kusonga mbele. 
(Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com simu namba-0712-727062)

Share on Google Plus

About Jestina George

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment