MAGUFULI NA KAMPENI ZA KUJIKOSOA, NAMFANANISHA NA MWALIMU NYERERE NA KAULI YA TUJISAHIHISHE

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Tiketi ya CCM Dkt John Pombe Magufuli

 Na Humphrey Pole Pole
Kumekuwa na maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia CCM, Dr. John Pombe Magufuli, kuibua na kuzungumzia mapungufu ya serikali ambayo yeye ni waziri. Baadhi ya watu wanaofuatilia kampeni zake wameenda mbali zaidi na kuhisi kuwa kwa kufanya hivyo, Magufuli anawafanyia kampeni labda bila yeye kujua wapinzani wake katika kinyang’anyiro cha Urais.
Bila shaka, kwa watu wenye mtizamo huo, kampeni za Magufuli zingekuwa zinatawaliwa na maneno yaliyoyajaa sifa nzuri za utendaji wa serikali na chama tawala. Kwa hiyo, kwa mtizamo huo, ni jambo la kushangaza kuona kuwa Magufuli anakosoa serikali aliyomo badala ya kuisifia na kuipamba majukwani. Kwa sababu hiyo, baadhi ya watu wanasema kuwa Magufuli anazungumza kama vile anagombea kupitia vyama vya upinzani.
Maoni ya namna hii pia yamekuwa yakielekezwa kwa katibu mkuu wa CCM, Ndg. Abdulrahaman Kinana, ambaye katika shughuli zake za kisiasa za chama chake katika maeneo mbalimbali hapa nchini amesikika mara nyingi akiikosoa serikali ya chama ambacho yeye ni katibu mkuu. Watanzania watakumbuka kuwa Ndg. Kinana aliwahi kuwaita baadhi ya mawaziri wa serikali hii 'mizigo' na kutaka wawajibishwe kwa kushindwa kutimiza wajibu wao kwa ufanisi. Kwa baadhi ya watu Ndg. Kinana hakufanya vizuri kuikosoa serikali yake hadharani na hasa kwa kuongea kama mpinzani.
Kitendo cha Magufuli na viongozi wa chama chake kuibua mapungufu na kuikosoa serikali yao hadharani inaonekana kama ni lugha ya wapinzani wa kisiasa. Hakika utamaduni huo ni sawa na kujikosoa mwenyewe. Hata hivyo, ili tuweze kuelewa kama kujikosoa ni jukumu pekee la vyama vya upinzani na wagombea wao, inabidi tujiruhusu kuelimishwa na maneno ya hekima aliyekuwa Rais na mpigania uhuru wa Guinea Bissau, kamarade, Amilcar Cabral ambaye alishawahi kusema kuwa kwa kiongozi au anayetaka kuwa kiongozi wa umma sharti awe na mwenendo wa kutoficha ukweli: Kwa maneno yake;
"Hide nothing from the masses of our people.Tell no lies.Expose lies whenever they are told. Mask no difficulties, mistakes, failures. Claim no easy victories."
Tafsiri yake ni kuwa, kiongozi asifiche chochote kwa wananchi. asiseme uongo, afichue uongo kila unapoibuka. Asifiche matatizo, makosa, mapungufu na kushindwa. Asijipe sifa nyepesi nyepesi.” Kutokana na hekima ya Amilcar Cabral ilivyoelezwa hapo juu, ni wazi kuwa anachofanya Magufuli ndicho haswa kinachotakiwa kufanyika. Kwa kufanya hivyo, Magufuli anaonyesha wazi kuwa anajua matatizo na mapungufu yaliyopo na badala ya kuyafunika na kuyapaka rangi anayaweka wazi. Bahati nzuri Magufuli amekuwa akielezea namna atakavyoshughulikia hayo matatizo na mapungufu. Bahati nzuri tabia hii ya Magufuli siyo mpya. Watanzania watakumbuka kuwa hulka hii ya Magufuli ilijionyesha wakati hata alipokuwa waziri chini ya Rais Benjamin Mkapa alipoikosoa Ofisi yake hadharani kwa baadhi ya watumishi wa ofisi hiyo kujimilikishia magari ya umma isivyo halali. Katika kipindi hiki cha kampeni, Magufuli amekuwa akitoa mapungufu ya serikali hata pale ambapo Rais Kikwete yupo.
Sambamba na Amilcar Cabral, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuandika kitabu mwaka 1962 kiitwacho "Tujisahihishe" akitaka Watanzania na hasa viongozi wawe tayari muda wote kujisahihisha. Katika kitabu hicho Baba wa Taifa, alisema kuwa “makosa ni makosa bila kujali ni nani ameyafanya. Muhimu ni kuyajua makosa hayo na kujisahihisha.” Katika kitabu hicho, Mwalimu Nyerere aliendelea kusema;
“Kujielimisha ni kujua ukweli wa mambo na kuwa na ujuzi wa sababu mbalimbali za mambo; na kama mambo hayo ni mabaya ni kujua jinsi ya kuyaondoa; na kama ni mema, jinsi ya kuyadumisha. Mpumbavu ni yule anayeyapa mambo sababu zisizo za kweli na kushauri dawa isiyo ya kweli katika kutafuta sababu za matatizo na jinsi ya kuyaondoa(Nyerere, 1962, 5).”
Kwa maelezo hayo ya Baba wa Taifa, ni wazi kuwa Magufuli ameamua kuwa mkweli katika kampeni zake na ameepuka kuwa mpumbavu kama alivyobainisha Baba wa Taifa.
Kujikosoa anakofanya Magufuli kunadhihirisha aina ya Rais tunayemhitaji. Itakuwa ni hatari kubwa kuwa na Rais asiyetayari kujikosoa au kukosolewa. Ni janga kubwa kwa nchi kuwa na Rais ambaye anaamini kuwa yeye ni mtakatifu asiyekosea. Rais wa namna hiyo ni lazima atakuwa ni dikteta na watakodhubutu kumkosoa na kuibua makosa yake watakiona cha moto. Kama historia za nchi mbalimbali inavyoonyesha, hili likitokea, Tanzania itakuwa katika dhahama kubwa.
Maandiko ya vitabu vitakatifu yanatuelekeza kuwa ukamilifu wa binadamu huja kwa kusimama katika ukweli, kujikosoa na kukubali kukosolewa na kuepuka hadaa. Vivyo hivyo, ukamilifu na uhai wa taasisi zinazoundwa na binadamu kama vile vyama vya siasa na serikali lazima viwe na uthubutu wa kujikosoa na kukubali kukosolewa kama anavyofanya Magufuli.
Kwa maelezo hayo hapo juu, ni ni wazi kuwa ukosoaji siyo jukumu pekee la vyama vya upinzani bali ni jukumu la kila mmoja hasa wale wanaotaka kuwa viongozi wetu. Hivyo, badala ya kumshangaa Magufuli kwa kubainisha makosa na mapungufu ya serikali ambayo yeye ni sehemu yake, tujielekeze katika kuwataka wagombea wengine katika nafasi mbalimbali waepuke hadaa na badala yake wafanye kampeni zao kwa kueleza ukweli.
Hadaa katika kampeni zitatupatia viongozi matapeli ambao bila shaka uongozi wao utakuwa wa hadaa kwa wananchi. Kinyume chake kiongozi mkweli na aliye na uthubutu wa kujikosoa anaonyesha kuwa ana uwezo wa kutafuta suluhisho la kweli la matatizo yaliyopo.
Kwa kuitimisha, Magufuli hajachemka katika kuikosoa serikali aliyomo bali, kwa kufanya hivyo, anaonyesha ufahamu wake wa hali halisi ilivyo. Zaidi, anaonyesha kuwa yeye ni mtu aliyetayari kusimamia ukweli jinsi ulivyo na hivyo ndivyo inapaswa kuwa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment