Lowassa: Nikishindwa urais nakwenda kuchunga ng’ombe

Mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na
By Julius Mathias, Mwananchi

Dar es Salaam. Mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa amesema akishindwa kupata ridhaa ya wananchi kuwa rais wa awamu ya tano ataenda kijijini kwake kuchunga ng’ombe.

Lowassa, kada wa muda mrefu wa chama tawala aliyetimkia upinzani na kufanikiwa kupitishwa kugombea akiviwakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ameyasema hayo alipofanya mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC Swahili) na kubainisha matokeo ya ushindani wowote lazima yawe na mshindi pamoja na aliyeshindwa.

"Nina ng’ombe wangu kijijini nitakwenda niwachunge na kuendelea na maisha," amesema Lowassa kwa kifupi alipoulizwa nini hatma yake endapo atashindwa kuukwaa urais kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumapili hii na kumpata kiongozi wa awamu ya tano.

Waziri huyo wa zamani, ameitumia nafasi hiyo kufafanua namna atakavyotekeleza sera ya elimu bure kuanzia shule ya msingi mpaka chuo kikuu na kubainisha vyanzo vya mapato atakavyovitumia.

Amezitolea mfano nchi za Ulaya ambazo zimefikia hatua hiyo kwa wananchi wake na kulinganisha na rasilimali ambazo Tanzania inazo kwamba zinatosha kufanya kile kinachofanywa na mataifa hayo ya magharibi na kuwapunguzia gharama Watanzania.

"Ulaya hakuna malipo yoyote yanayotozwa kwa wanafunzi. Tunazo rasilimali nyingi zinazotuwezesha kununua magari makubwa kama Range (Rovers) kwanini fedha hizo zisitumike kugharamia elimu? Tunayo hifadhi ya gesi iliyogundulika kusini nayo ni muhimu kwa uchumi. Watanzania wanipe ridhaa waone jinsi nitakavyotekeleza," amesema Lowassa.

Tofauti na chaguzi zilizopita, mwaka huu kumekuwa na mwamko mkubwa miongoni mwa wananchi hasa vijana ambao wamejitokeza na kushiriki kwa hatua zote za maandalizi yake kuanzia uandikishaji mpaka mikutano ya kampeni.

Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wapigakura waliojiandikisha na kuthibitishwa ni 22.75 milioni na miongoni mwao, katika kila watu 10 sita ni vijana hivyo kutoa changamoto kwa wagombea na vyama vya siasa kuweka mipango imara ya kulishawishi kundi hilo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment