Bunge jipya, mzigo zaidiBunge la Jamhuri ya muungano
By Nuzulack Dausen, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati ikisaka njia za kubana matumizi kuokoa fedha, Serikali ya Awamu ya Tano itakuwa na kazi ya kulipia gharama za uendeshaji zilizosababishwa na kuongezeka kwa wabunge 36 zaidi kwenye Bunge la Kumi na Moja lililopangwa kuanza Novemba 17 mjini Dodoma.

Tayari Rais John Magufuli ameshafuta safari za nje hadi kwa kibali maalumu, kuagiza Mamlaka ya Mapato (TRA) kukusanya kodi bila ya kupendelea, hasa kwa wafanyabiashara wakubwa, ikiwa ni hatua za mwanzo za kuhakikisha Serikali inapata fedha za kuiwezesha kujiendesha.

Lakini, utashi wa kuboresha utawala bora kwa kuongeza uwakilishi wa wananchi kwenye chombo hicho cha kutunga sheria uliilazimisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuongeza majimbo 26, ambayo yamesababisha kuongezeka kwa nafasi kumi zaidi za viti maalumu.

Kwa mujibu wa Ofisa wa Habari wa Bunge, Owen Mwandumbya, Bunge la 10 lililomalizika Agosti 21, lilikuwa na wabunge 357. Bunge hilo lilijumuisha wabunge 239 wa kuchaguliwa, viti maalumu (102), Baraza la Wawakilishi (5), wateule wa Rais (10) na Mwanasheria Mkuu (AG).

Hata hivyo, Bunge la Kumi na Moja sasa litakuwa na wabunge 393. Jumla hiyo inatokana na viti 264 vya majimboni, viti maalumu 113 kwa mujibu wa NEC, wateule wa Rais (10), Baraza la Wawakilishi watano na Mwanasheria Mkuu, George Masaju aliyeapishwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mpaka sasa Rais Magufuli hajateua mbunge yeyote katika nafasi zake 10, wakati bado majimbo manane hayajafanya uchaguzi kutokana na waliokuwa wagombea wa ubunge kufariki dunia.

Kuahirishwa kwa uchaguzi katika majimbo hayo, kumesababisha idadi ya viti maalumu vilivyosalia kuwa vitatu kati ya 113 vilivyowekwa na NEC kwa mujibu wa Katiba ambavyo mwaka huu vyama vya siasa vilikubaliana iwe asilimia 40 ya wabunge wa kuchaguliwa.

Kwa ongezeko hilo la wabunge 36, Serikali itahitajika kuongeza takriban Sh10.8 milioni kwa siku iwapo kila mbunge atalipwa Sh300,000 kwa siku za posho kwa viwango vya Bunge lililopita na iwapo mfumo wa malipo hautabadilishwa.

Ikumbukwe kuwa mapema Mei 6 mwaka jana, gazeti hili liliripoti kuwa Bunge hilo lilianza vikao vyake vya bajeti ya mwaka 2014/15 kwa posho mpya ya Sh300, 000 baada ya baadhi ya wabunge kutaka malipo hayo yaongezeke na kuwa sawa na yale waliokuwa wakilipwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

Jana, Ofisi ya Bunge haikuwa tayari kuweka bayana malipo ya posho kwa mbunge kwa siku, ikieleza kuwa posho na mshahara ni siri ya mbunge mwenyewe hivyo havitakiwi kuwekwa wazi kwa umma.

“Sheria zinakataza kuzungumzia masuala hayo. Masuala yoyote yanayohusu malipo ya wabunge wangeulizwa Hazina. Bila shaka Serikali imejiandaa vilivyo kumudu gharama hizo mpya,” alisema Mwandumbya.

Ukiachana na gharama hizo mpya, ongezeko la wabunge limelazimu maboresho kwenye ukumbi kwa kuongeza viti vitakavyotumiwa na watunga sheria hao wapya.

Mwandumbya alisema walichofanya ni kufunga viti vipya, vilivyokuwa vya akiba, katika mzunguko wa nyuma ndani ya ukumbi wa jengo hilo la kisasa lililozinduliwa mwaka 2006 na Rais aliyepita, Jakaya Kikwete.

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alisema walishindwa kufanya mabadiliko makubwa safari hii kutokana na muda baada ya kumaliza Bunge la 10 kuwa mdogo, lakini maboresho makubwa yanatarajiwa kufanywa siku zijazo.

Bunge la Kumi na Moja linatarajiwa kuwa moto kutokana na kambi ya upinzani kupata zaidi ya viti 100 vya wabunge wa majimboni na viti maalumu, hivyo kuwa na watu wengi zaidi wa kuweza kuibua na kujadili masuala ya kuibana Serikali.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment