HOJA ZA TEWUTA KWA TTCL SI SAHIHI


Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemus Mushi akizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam kujibu madai ya TEWUTA.

MNAMO tarehe 10 Novemba 2015, Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao wa Mawasiliano Tanzania TEWUTA kupitia kwa Katibu Mkuu wake Bw Junus Ndaro walizungumza na vyombo vy Habari. Katika mazungumzo hayo,TEWUTA ilitoa salamu za pongezi kwa ushindi wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli na Makamu wake kwa ushindi wao katika uchaguzi Mkuu wa uliofanyika Oktoba 2015. Aidha, TEWUTA ilitumia fursa hiyo kuelekeza tuhuma mbali mbali kwa Kampuni ya Simu Tanzania TTCL.
Kufuatia hatua hiyo, Menejimenti ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), inapenda kuujulisha Umma kuwa, madai yaliyotolewa na Chama cha TEWUTA dhidi ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL si sahihi.
Hoja za TEWUTA zimejikita katika upotoshaji wenye nia ovu ya kufanikisha malengo binafsi na kukwamisha jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wa TTCL wenye nia na malengo ya kutekeleza mpango mkakakti wa kuiboresha na kuiimarisha Kampuni ya Simu Tanzania.
Kwa uchache, Menejimenti ya TTCL inapenda kutoa taarifa sahihi kama ifuatavyo:
Kwanza, hali ya Kampuni ya simu Tanzania ni nzuri, utendaji wa kazi unaendelea vizuri, mahusiano ya kazi katika kampuni ni thabiti na jitihada mbali mbali za kuboresha huduma zinaendelea kwa ufanisi mkubwa.

Pili, Menejimenti ya TTCL inapenda kuujulisha Umma kuwa, hoja zote zilizotolewa na Chama cha TEWUTA si za kweli, ni taarifa zilizopotoshwa kwa makusudi, zikilenga kufanikisha malengo binafsi na kukwamisha jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Sayansi na Mawasiliano, Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni, Menejimenti na Wafanyakazi wa TTCL wenye lengo la kuifanya Kampuni kushamiri kibiashara na kutimiza kikamilifu Wajibu wake kwa Umma.
Tatu, Muundo wa mishahara ya Watumishi wa Kampuni ya simuTanzania TTCL uko wazi na ndio unaotumika kulipa mshahara ya wafanyakazi wote wa Kampuni ya Simu Tanzania. Ofisi inayolipa mishahara ya wafanyakazi wote wa TTCL iko idara ya Fedha na kusimamiwa na wafanyakazi wa Kampuni ya Simu. Hakuna Payroll yoyote ya Siri inayotumika tofauti na hiyo iliyoainishwa, hakuna posho zozote zinazolipwa kinyume na utaratibu.

Nne, kwa kuzingatia mabadiliko ya Kibiashara na Soko la Mawasiliano Menejimenti iliomba na kupata kibali cha Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL kumtafuta Mshauri mwelekezi kwa njia ya Zabuni ili kupitia na Kushauri TTCL juu ya Muundo wa Mpya wa Kampuni utakaoendana na Mahitaji ya Kibiashara na Soko.
Matokeo ya Kazi hii ya Mshauri mwelekezi yatabadilisha muundo wa Kampuni, Muundo wa Mishahara na Muundo wa utumishi wa Kampuni ya Simu Tanzania.
Meneja Uhusiano wa TTCL, Nicodemus Mushi akizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam.
Tano, Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Simu Tanzania TTCL imekuwa na mchango mkubwa sana katika kusukuma maendeleo ya TTCL chini ya uenyekiti wa Dr. Enos Bukuku na baadae chini ya Mwenyekiti wa muda Mhe. Judge Joseph Sinde Warioba. Mambo mengi yametekelezwa chini ya Bodi hii yakiwemo Uendeshaji na usimamizi wa mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Kuondoka kwa Mbia Mwenza Bharti Airtel, Utekelezaji wa Mradi wa mabadiliko ya mfumo wa kibiashara (Transformation project) kusukuma jitihada mbali mbali za kuipatia Kampuni mitaji ya kuiwezsha kufanikisha mipango yake kwa wakati.
Sita, Kampuni ya Rubiem ni Mshauri mwelekezi aliyepatikana kwa kufuata taratibu sahihi za manunuzi ya Umma. Mchango wa kampuni hii katika mpango wa mageuzi ya kibiashara ya kampuni ni mkubwa na unaonekana dhahiri. Matokeo ya kazi yake yataanza kuonekana mwishoni mwa mwaka huu ambapo huduma na bidhaa mpya zitaingia sokoni. Mshauri huyu anatarajia kukamilisha kazi yake katika robo ya kwanza ya mwaka 2016. Ieleweke pia kwamba, hatua ya Menejimenti kumuongezea muda mshauri huyu hazihusishi gharama zozote za nyongeza nje ya mkataba wake wa kazi na TTCL.
Kutokana na ufafanuzi huu, tunaomba Umma kupokea taarifa hizi sahihi na kuendelea kuipa ushirikiano Kampuni yao ya Kizalendo ili iweze kuwahudumia kwa ufanisi zaidi. Tunawakikishia Wateja wetu wote wa ndani na nje ya nchi huduma bora zaidi,za uhakika na  kwa gharama nafuu.
TTCL- HULETA WATU KARIBU.
Imetolewa na Idara ya Uhusiano,
TTCL Makao Makuu,

DAR ES SALAAM.
Share on Google Plus

About Jestina George

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment