WAZIRI MKUU MAJALIWA AONGOZA MBIO ZA HAPA KAZI TU DODOMA HALF MARATHON

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongoza mbio za Wabunge za Hapa Kazi Tu Dodoma Half Marathon zilizoanzia Bungeni hadi uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Januari 30, 2016. Kushoyo kwake ni Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt Tulia Ackson. Mwansasu (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya Washiriki wa mbio za Hapa Kazi Tu Dodoma Half Marathon wakishiriki mbio hizo mjini Dodoma Januari 30, 2016.
Mmoja wa wapigapicha walioshiriki mbio za Hapa Kazi Tu Dodoma Half Marathon alilazimika kuomba msaada kwa askari wa usalama barabarani Mjini Dodoma Januari 30, 2016. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi ufunguo wa pikipiki mshindi wa kwanza wa mbio za Hapa Kazi Tu Dodoma Half Marathon upande wa wanaume, Emmanuel Giriki kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Januari 30, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi zawadi ya Pikipiki mshindi wa kwanza upande wa wanawake wa Mbio za Hapa Kazi Tu Dodoma Half Marathon, Angela Davile (kulia) kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Januari 30, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Benki ya CRDB tawi la Dodoma ambao wamedhamini pambano la mpira wa miguu kati ya wabunge na benki hiyo kwenye uwanja wa Jamhuri Januari 30,2016. Benki hiyo pia ilitoa vifaa vya michezo kwa timu ya Bunge. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuandaa kikao cha haraka na viongozi wa vyama vya michezo nchini ili wamueleze kila mmoja amejipanga vipi kuinua viwango vya michezo katika chama chake.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumamosi, Januari 30, 2016) wakati akizungumza na mamia ya viongozi na wakazi mbalimbali wa mkoa wa Dodoma ambao walishiriki mashindano ya mbio za nusu marathon (km. 21 na km. 5) zilizofanyika leo mjini Dodoma.

Mashindano hayo yalijulikana kama “HAPA KAZI TU HALF MARATHON” yamefanyika ikiwa ni sehemu ya kuhimiza uchapakazi miongoni mwa Watanzania lakini pia ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kuadhimisha siku 100 za utendaji kazi tangu Rais John Pombe Magufuli alipoapishwa na kuanza kazi.

“Kuna maboresho yanaendelea ndani ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo lakini haya yote hayawezi kufanikiwa kama viongozi wa michezo hawajajipanga vizuri. Ninatakata niandaliwe kikao cha siku moja na viongozi wa vyama vya michezo nchini ili waje wanieleze kila mmoja amejipanga vipi kuinua hali ya mchezo wake,” alisema huku akishangiliwa.

Alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania kwa kuandaa mbio hizo muhimu za kuhimiza Watanzania kuchapa kazi, lakini pia ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kushiriki katika mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika baadaye mwaka huu huko Rio de Janeiro, Brazil.

“Tunataka tuondokane na kauli ya Tanzania kuwa ni kichwa cha mwendawazimu na nipende kusisitiza kuwa maandalizi haya yasiwe ya mwisho bali yawe ya muda mrefu kwa sababu tunaenda kushiriki mashindano ya dunia. Nasema tena, tuache utamaduni wa maandalizi ya kukurupuka,” alisisitiza. 

Aliwataka wadau mbalimbali wajitokeze kusaidia taasisi za michezo.

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alishiriki mbio za km. 2.5 kuanzia saa 1 asubuhi, alikimbia kutoka eneo la Bunge hadi uwanja wa Jamhuri na kuzindua mashindano ya km. 21 saa 1:47 asubuhi na yale ya km. tano aliyazindua saa 1:51 asubuhi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alikabidhi pikipiki aina ya GSM kwa washindi wa kwanza wa nusu marathon, mabati 100 kwa washindi wa pili na mabati 40 kwa washindi wa tatu. Mshindi wa tatu hadi wa 10 kwa wanawake na wanaume walikabidhiwa fedha taslimu.

Washindi wa kwanza hadi wa tatu waliokabidhiwa zawadi na Waziri Mkuu upande wa wanawake ni  Anjelina Daniel (Pikipiki); Fadhila Salum (mabati 100) na Catherine Lange (mabati 40). Wote wanatoka mkoa wa Arusha. 

Kwa wanaume walioshinda nafasi kama hizo ni Emmanuel Giniki (Katesh, Babati) aliyeshinda pikipiki; Gabriel Gerald wa Arusha (mabati 100) na Fabian Joseph wa Arusha (mabati 40).

Wakati huo huo, Benki ya CRDB Dodoma ilitoa zawadi za sh. 250,000/- kila mmoja kwa washiriki watatu ambao ni walemavu walioamua kushiriki mbio hizo mwanzo hadi mwisho. Waliokabidhiwa zawadi hizo na Waziri Mkuu ni Bw. Hassan Hussein Sharif, Bw, Christian Ally Amour na Bw. Shukuru Khalfani.

Benki hiyo ilikabidhi pia vifaa vya michezo kwa ajili ya timu ya wabunge kwa ajili ya pambano la soka linalotarajiwa kufanyika leo saa 10 jioni kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma baina ya timu ya Bunge na timu ya CRDB. 
Share on Google Plus

About JG Blog Team

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment