RAIS MAGUFULI SI MKWAPUAJI BALI NI MTEKELEZAJI
Na Emmanuel J. Shilatu

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema Rais Magufuli ni mkwapuaji wa sera za Chadema lakini hana uwezo wa kuzitekeleza kwa vitendo kwani anatokana na chama chenye misingi ya wizi na Serikali yake haiwezi kuwa safi na ataishia kufanya maigizo ya utumbuaji majipu!!

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Chadema Visenti Mashinji wakati akifungua kongamano la Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) na Umoja wa Wana Chadema Vyuo Vikuu (CHASO) mjini Dodoma. 

Maana nyepesi ya neno “Mkwapuaji” ni mporaji ambapo Chadema wanataka kuuaminisha umma kuwa anachokifanya Rais John Pombe Magufuli kimetoka hewani ama ni sera zao lakini wanasahau Magufuli ameingia Ikulu kutokana na kufaulu kunadi vyema mkataba na Wananchi ujulikanao kama Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambazo ndizo sera zenyewe anazozitekeleza leo hii. Hapo utasemaje Magufuli ni mkwapuaji wa sera za Chadema zilizokataliwa na Wananchi kupitia sanduku la kura na kuacha kutekeleza sera za chama chake (CCM)  zilizokubaliwa na kumpeleka Ikulu?

Chadema wanajivika joho la wapambanaji wa ufisadi nchini angali midomo yao imejaa punje za ufisadi. Tuweke kumbukumbu sawa katika kulithibitisha hili; Chadema wanapokea ruzuku ya takribani Tsh. Milioni 500 kwa kila mwezi toka kwa ofisi ya msajili wa vyama vya kisiasa nchini! Lakini leo hii wanashindwa hata kuwa na ofisi za vyama vyao iwe ni mikoani, wilayani au hata kwenye kata na hao hao ndio watu wanaopokea mamilioni ya pesa kila mwezi na hao hao hawaonyeshi kwa jamii matumizi ya pesa hizo. Pesa hizo zinapokwenda hazijulikani, hapo watajiitaje wapambanaji wa ufisadi nchini wakati wao wenyewe ni lebo ya ufisadi? 

Weka pembeni hilo la ruzuku, tumulike zile pesa za msaada wanazopewa na mfadhili wao ambaye ni mfanyabiashara mkubwa Mustapha Sabodo ambapo aliwapa pesa za kuchimba visima kwenye kila jimbo lenye mbunge wa Chadema, akawapa  pesa za ujenzi wa ofisi ya makao makuu ya Chadema lakini mpaka leo hakuna cha ofisi wala kisima kilichochimbwa. Wanapata wapi ujasiri wa kujiita wapambanaji wa vita ya ufisadi wakati ndani mwao kumejaa “Panya” wanaotafuna pesa kama mchwa? Hiki kweli utakiita chama kinachopinga vita ufisadi ama ni Saccoss ya kufa na kuzikana?

Ukweli unabaki pale pale kwamba CCM ndio waasisi wa vita ya mapambano ya ufisadi nchini na anayoyafanya Rais Magufuli kwa sasa ya kupambana na ufisadi nchini kwa kuyatumbua majipu mafisadi yote ni mwendelezo wa urithi toka kwa Marais ama toka kwa Serikali zilizopita.
Kwa wale wasioelewa Kwenye katiba ya CCM kifungu cha 1 ibara ya 8(2) inatoa masharti kwa kila mwanachama kuwa mtu anayefanya juhudi za kuielewa kuieleza na kuitekeleza itikadi na siasa ya CCM. Hivyo mojawapo ya kazi ya mwana CCM ama kada wa CCM ni lazima awe mstari wa mbele katika mapigano dhidi ya ufisadi na mafisadi nchini. Hii haijalishi awe anatoka katika kamati kuu (C.C) ama katika tawi. 
Serikali imekuwa ikisikiliza kupokea na kutimiza wajibu wa utekelezaji wa mambo yote yahusuyo rushwa na ufisadi nchini kupitia kwa “makomandoo” mbalimbali wa upiganaji wa maovu nchini. 

Tusisahau jinsi gani Chifu Abdallah Fundi Kira alivyochapwa voboko kutokana na kupokea rushwa ya sh. 25/-. Pia wahujumu uchumi hawatakaa wamsahau Edward Sokoine kwa jinsi alivyopambana nao. Haya ndio mapambano ya dhahiri nay a ushahidi wa Serikali za CCM.

Tusimsahau Mzindakaya ‘Mzee wa Mabomu’ alivyomlipua Idd Simba kwenye sakata la sukari. Pia tumkumbuke Sokoine na machukizo dhidi ya wahujumu uchumi. Pia tusimsahau Dr. slaa alipojitoa muhanga kuwataja mafisadi (10 list of shames) wa EPA pale Mwembe Yanga. Tuendelee kukumbuka harakati za mapigano ya Dialo dhidi ya uwekezaji ndani ya maliasili. 

Yapo mambo mengi mno yaliyoibuliwa na baadhi ya wanaharakati lakini nayo Serikali haipo nyuma kwenye uchukuaji wa utekelezaji wa dhahiri wa mapigano dhidi ya ufisadi bila ya kuangalia hadhi, umaarufu wala wadhifa wake. Pia tumeshuhudia viongozi waandamizi na makada wakubwa wa chama wakijiuzulu na wengine kulala rumande na hata kupelekwa mahakamani. 

Ila sisi wananchi tu wepesi sana wa kusahau. Tusisahau kukumbuka jinsi gani watuhumiwa wa EPA wanavyopandishwa mahakamani pia tu mashuhuda wa jinsi gani vigogo wa BOT walivyosota jela kwa ajili ya kashfa za magendo pacha, uzidishaji wa utengenezaji wa noti EPA. Jamii pia imeshuhudia watuhumiwa wa nyara za Serikali za kontena lililokuwa na meno ya tembo waliburuzwa mahakamani  

Tusisahau sakata la minofu ya samaki na kitita cha sh. Million 900 kule Mwanza akina Mzindakaya na Lamwai walimpelekea kilio Profesa Mbilinyi hatakaa alisahau hili. Pia tukumbuke dhoruba iliyompata Aron Chiduo enzi ya utawala wa Mwinyi. 

Kwa haya, napenda kuzipongeza Serikali zote kwa kuonyesha uhai kwenye mapigano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini. 

Naam, mtu akifanya vizuri lazima apewe haki (pongezi) zake tena kwa roho moja. Wale wanaobeza harakati hizi sijui tuwaweke kundi gani ambalo jamii itawaelewa. 

Ni jambo la kushangaza kuona ni jinsi gani watu ama kundi la watu linavyojipa sifa ambazo sio zao. Mathalani vyama vya upinzani wanajitutumua kwa kauli zao kwamba wao ndio waanzilishi wa mapambano ya rushwa na ufisadi nchini. 

Rais Magufuli naye pia ameendeleza mapambano yale yale ya vita dhidi ya rushwa na ufisadi nchini kwa kuyatumbua majipu sugu wale wote watafunaji wa rasilimali za Taifa na watumiaji madaraka vibaya kwa maslahi binafsi. Tumeona vigogo wazito kabisa wakikumbwa na tumbua majipu ya Rais Magufuli pasipo uonevu wala kumuonea haya mtu kwani haya ndio matarajio ya Watanzania walio wengi kuona yakitendeka. Kama ni upele umempata mkunaji, John Pombe Joseph Magufuli.

Tumekuwa Taifa la watu vigeugeu na wapotoshaji, leo hii waliokuwa wakipiga kelele juu ya mafisadi na watu wanaotumia madaraka vibaya kuwa hawashikiki ndani ya nchi , leo hii watu wale wale waliokuwa wakipaza sauti za kuona mapambano ya vita ya ufisadi nchini ndio wamegeuka watetezi wa mafisadi wenyewe.

Rais Magufuli ameendelea kujionyesha kwamba yeye ni mtendaji haswaa kwani alihaidi kukusanya kodi na kuziba mianya yote ya ukwepaji kodi ili tuondokane na tatizo la utegemezi na kuwa ombamba. Leo hii tunayaona matunda ya utekelezaji wake kwani mapato ya ndani ya nchi yameongezeka kutoka makusanyo ya Bilioni 800 kwa mwezi na hadi kufikia makusanyo ya trilioni 1.5 kwa mwezi. Huu ni ushahidi wa utekelezaji na utendaji aliojaaliwa Rais Magufuli.

Rais Magufuli huyu huyu alihaidi kubana matumizi ya pesa nchini na amekuja kuyaishi maneno yake kwani leo hii amefanikiwa kufuta posho za ovyo ovyo walizokuwa wanalipana vikaoni, amefuta safari za nje za viongozi wote na kusafiri ni mpaka upate kibali rasmi, amefanikiwa kuwafuta watumishi hewa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara pia amefuta walsha na semina zisizo na tija na badala yake watu wanatakiwa wafanye kazi tu kwa vitendo na porojo. 

Haya mambo yote yameendelea kuimarisha mapato ya ndani ya nchi na pesa nyingi zimeendelea kuokolewa. Mathalani hivi karibuni Bunge walifanikiwa kuokoa bilioni 6 fedha walizozikabidhi kwa Rais Magufuli na yeye kuzielekeza zikatengeneze madawati na hivyo kutaondoa tatizo la madawati nchini. Nani kama Magufuli?

Jambo la kufurahisha Rais Magufuli ameonyesha si mkwapuaji wa Sera za chama chochote kile bali anasimamia sera za chama chake na kuonyesha kwa matendo utumishi na uwajibikaji wa dhati; Rais Magufuli huyu huyu ameongeza makusanyo na ameonyesha uwazi katika kutoa taarifa kila mwezi juu ya mapato na matumizi ya makusanyo ya pesa yanayofanywa na Serikali. Mpaka sasa Rais Magufuli amejionyesha si mkwapuaji bali ni mtekelezaji, mtendaji, Mzalendo na mchapa kazi mwenye maono na malengo ya kutuondoa kwenye umaskini.

0717488622
Share on Google Plus

About Jestina George

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment

Note: only a member of this blog may post a comment.