WATUMISHI 105 KUPELEKWA OFISI ZA BALOZI NJE YA NCHI NA WATUMISHI 79 KUREJESHWA NCHINI

Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa imejipanga kuwapeleka kwenye Balozi zake nje Watumishi wapatao 105 na kuwarejesha nchini wengine 79 ambao miongoni mwao muda wao wa utumishi balozini (Tour of Duty) umemalizika na wengine kustaafu kwa mujibu wa sheria za Utumishi wa Umma. Kwa kawaida tour of duty kwa Watumishi nje ni ya muda wa miaka minne (4).

Tanzania ina Balozi 35 nje ya nchi ambazo kwa ujumla wake zina Watumishi 234. Miongoni mwa Watumishi watakaorejea nchini wamo Mabalozi, Maafisa, Wahasibu na Makatibu Muhtasi.

Hadi sasa Mabalozi waliorejea nchini ni watatu (3) ambao ni Balozi Peter Kalaghe aliyekuwa Uingereza, Balozi James Msekela aliyekuwa Italia na Balozi Batilda Burian aliyekuwa Japan.

Itakumbukwa kuwa, Januari 25, 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja Mabalozi hao ambao mikataba yao iliisha na wengine kwa ajili ya kupangiwa majukumu mengine.
Aidha, jumla ya Watumishi tisa  wa kada mbalimbali waliokuwa Balozini wamerejea nchini hadi sasa na wengine wanaendelea kurejea kulingana na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha jukumu hilo.

Utaratibu wa kuwapeleka na kuwarejesha Watumishi Balozini ni wa kawaida na upo duniani kote kwa mujibu wa sheria za kimataifa ukiwemo Mkataba wa Vienna unaotoa mwongozo kwenye masuala ya kidiplomasia.

Wizara itaendelea kupeleka Watumishi wenye sifa na tija kwa taifa ili kuiwakilisha nchi kikamilifu.

WAKATI HUOHUO, Waziri wa Viwanda na Biashara wa Oman Mhe. Dkt. Ali Bin Masoud Al Sunaidy alifanya ziara  ya kikazi nchini Tanzania kuanzia tarehe 12 April hadi 14 April, 2016.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni  kushiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Oman, kongamano hili lilikuwa na kauli mbiu ya ‘’ Oman Tanzania Road show : Exploring Opportunities in Investment and Business between Tanzania and Oman’’.

Ziara na kongamano hili  imelenga zaidi katika sekta za Madini, Kilimo na uboreshaji wa mazao ya Kilimo, Mifugo, Miundombinu na Mawasilisno, Uvuvi, Usafirishaji, Utalii, Petroli na Gesi. Mgeni Rasmi katika kongamano hili alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan

Katika ziara hii, Mhe. Waziri Al Sunaidy aliongozana na ujumbe wa watu 108 ambapo 12 walikuwa ni Maafisa kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali ya Oman na wengine waliobaki kutoka Sekta Binafsi kutoka nchi hiyo kwa lengo la kukutana na Taasisi kama hizo hapa nchini.

Kwa upande wa Tanzania wafanyabiashara 190 walishiriki na wenzao kutoka Oman katika kongamano na baadae katika mikutano ya ana kwa ana (Business to Business meetings).

MAFANIKIO YA ZIARA

1.Wakati wa ziara hiyo, Tanzania na Oman zilisaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya Tanzania Chambers of Commerce  na Oman Chambers of Commerce wa kuanzisha Kampuni ya Oman Tanzania Investment Company (OTIC). Kampuni imeanzishwa kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji Tanzania na Oman na imeazimia kuanza na mtaji wa Dola za Marekani milioni 25 ambazo zitatumika kutoa mikopo kwa wawekezaji ;

2.Serikali ya Oman imeonesha nia ya kuwekeza katika kiwanda cha Sukari cha Kagera (Kagera Sugar) na kukipa uwezo wa kuzalisha tani 400,000 ambazo zitauzwa katika soko la Tanzania. Uzalishaji huu pia utahusisha uzalishaji wa Umeme, spiriti na hamira  itokanayo na mabaki katika kuchakata sukari. Umeme utaingizwa katika gridi ya Taifa wakati spiriti ambayo ni muhimu katika matumizi ya tiba itauzwa katika masoko ya ndani na nje ya Tanzania. Aidha, Oman inahitaji hamira ambayo inahitajika kwa kiasi kikubwa nchini humo na nchi zingine za mashariki ya kati ;

3.Mbali na uzalishaji wa sukari, Serikali ya Oman pia inakusudia kuingia ubia na Kagera Sugar katika kilimo cha umwagiliaji cha uzalishaji wa mazao ya chakula kwa ajili ya matumizi ya Oman na Tanzania. Utekelezaji wa miradi hii utaleta faida kwa Tanzania ikiwa ni kuongeza uzalishaji wa sukari na hivyo kupunguza pengo kati ya uzalishaji na mahitaji halisi ya sukari, lakini pia unategemea kuzalisha nafasi zaidi ya 5,000 za ajira na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira ;

4.Serikali ya Oman pia ilionyesha nia yake ya kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika mradi wa uboreshaji na upanuzi wa bandari ya Tanga lakini pia kuziwezesha bandari za Tanzania kuwa na ushirikiano na zile za Oman ;

5.Wawekezaji kutoka Oman pia wameonyesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa nyumba za kisasa mkoani Mtwara ili kuondoa tatizo la makazi stahili kwa watendaji wakuu wa makampuni ya mafuta na shughuli zinazoendana na sekta hii ambao hulazimika kila siku kusafiri kwa ndege kutoka Dar Es Salaam kwenda Mtwara na kurudi jambo ambalo lina gharama kubwa pamoja na ombi la ekari 1,000 kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga na maua;

6.Wawekezaji kutoka Oman pia wameonyesha nia ya kuwekeza katika maeneo kadhaa ikiwemo uzalishaji wa mitamba na chakula cha mifugo huko Mivumoni, Tanga, ranchi na machinjio ya Ruvu, miundombinu na viwanja vya ndege, ujenzi wa nyumba za kisasa  Kigamboni na Zanzibar pamoja na miradi mingine katika sekta ya utalii  pamoja na kuwekeza katika sekta ya viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na mifugo ;

7.Wafanyabiashara wa Tanzania wamepata nafasi ya kutambua fursa zilizopo Oman ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa soko kwa bidhaa za chakula kama vile matunda, nyama, unga, sukari, hamira nk; na

8.Tanzania kwa ujumla ilinufaika kwa kutangaza fursa za uwekezaji ambazo zipo katika sekta zinazolengwa na wawekezaji wa Oman lakini pia kubaini fursa zilizopo Oman ambazo wafanya biashara wa Tanzania wanaweza kunufaika nazo pamoja na kuwaunganisha wafanya biashara wa Tanzania na wenzao wa Oman katika kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi zetu.

Hivyo, utekelezaji wa matarajio haya unategemea kuongeza ajira, kuongeza ubora na thamani ya mazao ya kilimo na kutanua wigo wa masoko kwa bidhaa za Tanzania na pia kukuza sekta ya viwanda nchini.

Imetolewa na:
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa 
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment