KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII AZINDUA JARIDA MAALUMU LA TAASISI YA WANYAMAPORI PASIANSI JIJINI MWANZA.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi (wa kwanza kushoto), hii leo akizindua Jarida Maalumu la Taasisi ya Taaluma za Wanyamapori Pasiansi (Pasiansi Wildlife Training Institute), iliyopo Jijini Mwanza. Shughuli hiyo imeambatana na Uzinduzi wa Makala Maalumu ya Miaka 50 ya taasisi hiyo.

Na BMG
Serikali imeahidi kuendelea kuijengea uwezo Taasisi ya Taaluma za Wanyamapori iliyopo Pasiansi jijini Mwanza, ili kukabiliana na matukio ya ujangili ambayo yametikisa nchi miaka ya karibuni.

Akizungumza na wanahabari katika uzinduzi wa Makala Maalumu ya Maadhimisho ya miaka 50 na Jarida Maalum la taasisi hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, amesema taasisi hiyo imetoa mchango mkubwa katika kufundisha askari wanyamapori ambao wamesaidia kwenye vita dhidi ya ujangili na kupunguza matukio ya ujangili nchini.

Meja Jenerali Milanzi amesema katika miaka ya karibuni Tanzania imetikiswa na matukio ya ujangili ambayo yamesababisha kuuawa kwa wanyamapori wakiwemo tembo na kuhatarisha uwepo wa wanyama hao ambao ni kivutio kikubwa cha watalii.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa Taasisi ya Wanyamapori Pasiansi na vyuo vingine, serikali itaendelea kuvijengea uwezo wa kifedha na rasilimali watu ili vitoe taaluma inayoendana na mahitaji katika kukabiliana na matukio ya ujangili.

Mbali na kuvijengea uwezo vyuo hivyo, Meja Jenerali Milanzi, amesema serikali pia inatambua umuhimu wa wananchi wanaoishi kuzunguka maeneo ya hifadhi na kwamba itaendelea kuwaelimisha wananchi hao ili washiriki kikamilifu kwenye vita dhidi ya ujangili.

Taasisi ya Taaluma za Wanyamapori Pasiansi (Pasiansi Wildlife Training Institute) ilianzishwa mwaka 1966 hivyo kesho june 15,2016 inatarajia kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.
Share on Google Plus

About Jestina George

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment