Agosti 10 2016....Naikimbiza DEATHDAY kuliko kuikimbia BIRTHDAY

Na Mubelwa T Bandio
Ni Agosti 10, 2016...Kwangu, mwaka mwingine unaadhimishwa maishani mwangu hii leo.
Ndio.....
Wengine wanaona kama siku ya kusherehekea maisha, kwangu ni ya KUADHIMISHA maisha zaidi.
Hakuna anayepatia katika kusherehekea na / ama kuadhimisha, lakini kwangu, Agosti 10 huwa ni AKISI ya maisha yangu kwa muda wote ambao nimeyajua.
Kuangalia nyuma namna ambavyo nimekuwa sehemu ya matatizo na suluhisho kwa jamii pendwa niishiyo.
Naakisi kuona nimegusa maisha kiasi gani na ni kiasi gani nachangia jamii yangu kuwa vile ambavyo napenda iwe.

MAISHA. Nimejifunza kuwa hayako sawa. Na naamini huo ndio usawa wake, kwani humu tuishimo hakuko sawa.
Hivyo, haitakuwa sawa kwa maisha kuwa sawa katika "uwanja" usio sawa kwa waishimo.
Na...
Najua nililoanza nalo na nitakaloendeleza halitaeleweka sawa, na huo ni udhihirisho wa usawa wetu, ambao nao hauko sawa.
Kwa wewe unayesoma hapa hivi sasa, ni kwa kuwa "umekua" na kufikia umri wa kusoma na kuelewa. Huu ni umri wa kusherehekea ama kuadhimisha siku kadhaa za kuzaliwa kwako.
Na, kama unasoma hapa, jambo moja ninaloweza kukuhakikishia ni kuwa UTAKUFA.
Kwa hiyo, kama wanadamu, haya mawili yanakuwa ya lazima. Ukizaliwa, utakufa. Tofauti ya maisha yetu ipo katikati ya haya mawili.
Kama nilivyowahi kuandika, kuwa  UTAKUMBUKWA KWA DESHI YA MAISHA YAKO (rejea hapa)
Maishani, nimehudhuria BIRTHDAY(s) na MISIBA mingi tu, na kote nimejifunza mengi kuhusu maisha yetu ya sasa, maisha tunayoyataka na hata namna tunavyojitahidi kuifikia TAMATI ya maisha yetu.
Labda funzo kuu nililowahi kushiriki nanyi ni lile nililoliandika  HAPA Agosti 22, 2011 baada ya kuhudhuria msiba wa Dada yetu hapa Washington DC.
Maisha yetu ya sasa yanaonekana kuwa ya mchakamchaka, twayakimbiza matumaini na (katika hali ya kushangaza) hata siku zaonekana kuwa fupi kuliko awali. 
Kabla hujajipanga, ni kesho, ni juma lijalo, ni mwezi ujao na mwaka bila kukamilisha mengi uliyoamini ungependa kuyakamilisha katika muda uliojipangia.
Ninapoangalia miaka hii niliyoishi, naiona kuwa mingi sana. Si kwa kuwa nimeishi mingi kuzidi wote, bali kwa kuzingatia ni mara ngapi nimekuwa nikiamini nimefika mwisho wa uhai.
Nakumbuka kusoma makala ya Kaka Eric Shigongo, iliyosema kuuona mwaka mpya ni nafasi ya ziada. Na naamini katika hilo.
Mara kadhaa (na ni zaidi ya moja) nimekuwa kwenye nafasi ya kuona kama kesho ilikuwa mbali na isiyofikika kwangu nikiwa hai. Siku ambayo hunijia akilini zaidi juu ya hilo, ni HII
Lakini leo wewe unasoma nililoandika kwa kuwa nilipata NAFASI YA ZIADA MAISHANI kutumia karama niliyokabidhiwa na Mwenyezi Mungu, kuboresha maisha ya kila niwezaye. 
NI NAFASI YA ZIADA katika kuikimbiza "siku ya mwisho"
Nikirejea kwenye kichwa cha bandiko hili,fikra kwamba maisha yetu ya sasa ni kama kuikimbiza kesho kuliko kuifikiria leo na hata jana, kunatufanya tuonekane kuyawaza yajayo kuliko tulikotoka.
Ni hili linalonifanya niamini kuwa, maisha yetu ya sasa yamewekeza katika yajayo. Na kama nilivyoeleza kabla, jambo pekee ambalo sote tuna hakika nalo, ni kifo.
Na ndio maana nikasema, MAISHA ya sasa. Ni kukimbiza DEATHDAY kuliko kuikimbia BIRTHDAY
Anyway!
Nisijesahau kujitakia EARTHday njema.
Najua fika kuwa hongera na shukrani za maisha yangu nazipokea kwa sababu ni Mungu aliyeniweka hai mpaka sasa. 
Na ndiye aliyenipa WAZAZI wangu ambao sina ninanloweza kueleza kuhusu nafasi yao maishani ikalingana na walilotenda.
Labda jambo moja tu, kwamba walinibariki na NDUGU ambao uwepo wao umekuwa kama egemeo la kukua kwangu. Hawa ndugu wameniwezesha kuambatana na JAMAA ambao kwa muongozo wa ndugu, wameniwezesha kuwa nilivyo. Si unakumbuka kuwa  Twachagua maongezi, maongezi yachagua mawazo na mawazo yatuchagulia jamii? (Isome hapa) 
Nina maRAFIKI ambao wananisaidia katika kukua kwangu. Hawa nawajumusha na wale wanajiona kama maadui kwangu, ambao mara nyingi wamenifanya kujitahidi kukamilisha mambo ili wasipate la kusema.
Hahahahahaaaaaaaaaaaaaaaa
Kipekee, namshukuru mke wangu mpenzi Esther na wanangu Paulina na Annalisakwa kuwa wavumilivu kwenye harakati zangu (nyingine hazielewekagi yaani)
Zaidi, wale waliochangia nikawa nilivyo katika fani. Na washirika wangu wakuu katika kazi, Dj Luke Joe na Harieth Shangarai, ambao "njaa tugangayo" kutimiza WAJIBU wetu kwa jamii, twaijua wenyewe.
Upendo mkuu kwenu
Hahahaaaaaaaaaaaaaa
Ni siku nyingine ya kukumbuka kuzaliwa kwangu. Nalikaribia hitimisho la maisha, na nikilijongelea, najitahidi kukamilisha dhumuni yangu ya kuwa humu duniani.

Mungu atubariki na kutuonyeshe namna muafaka ya kutenda kila lililo jema, kadhi tuukaribiavyo mwisho wetu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment