Pangani nzima kupatiwa umeme ifikapo 2018 : Kuwa wilaya ya mfano Tanzania kwa vijiji vyote kuunganishiwa na umeme

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mkaramo kilichopo wilayani Pangani mkoani Tanga. Waziri Muhongo yupo mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua miradi ya kusambaza umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na kuzungumza na wananchi. Wananchi wa kijiji cha Sakula kilichopo wilayani Pangani mkoani Tanga wakionyesha mabango yenye jumbe tofauti mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) walipomsimamisha njiani kwa lengo la kuwasilisha kero mbalimbali wakati akielekea katika kijiji cha Mkaramo kwa ajili ya kuhutubia wananchi 
Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainab Abdallah Issa (kushoto) akiwasilisha mahitaji ya umeme katika wilaya ya Pangani 
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisisitiza jambo wakati alipokuwa akiwahutubia wakazi wa kijiji cha Mkaramo kilichopo wilayani Pangani mkoani Tanga (hawapo pichani) 
Waziri wa Nishati na Madini (kulia) akipokea kero mbalimbali kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Mkaramo 


Na Greyson Mwase, Pangani 

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa Serikali ina mpango wa kusambaza nishati ya umeme katika wilaya nzima ya Pangani na kuifanya kuwa wilaya ya mfano ndani ya kipindi cha miaka miwili. 

Profesa Muhongo aliyasema hayo alipokuwa akihutubia katika kijiji cha Mkaramo kilichopo wilayani Pangani mkoani Tanga. Profesa Muhongo yupo mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). 

Kabla ya kuwasili katika kijiji hicho msafara wa Profesa Muhongo ulisimamishwa na wananchi wa kijiji cha Sakura kilichopo wilayani Pangani mkoani Tanga waliokuwa na mabango wakiomba kupatiwa umeme katika kijiji chao. 

Akizugumza kwa niaba ya wanakijiji wenzake, Boga Mbega alisema kuwa kijiji hicho kimekuwa gizani kwa muda wa miaka mingi hali inayopelekea uchumi katika kijiji hicho kudumaa. 

Aliongeza kuwa kutokana na ukosefu wa umeme katika kijiji hicho wamekuwa wakifuata huduma za jamii kama vile matibabu na maji katika vijiji vya mbali na hivyo kuhisi kama wako kwenye kisiwa cha giza. 

Mara baada ya Waziri Muhongo kuwasili katika kijiji cha Mkaramo na kuanza kuhutubia alisema kuwa kutokana na wilaya ya Pangani kuwa nyuma kimaendeleo kuliko wilaya nyingine nchini, Serikali imepanga mikakati ya kuhakikisha kuwa wilaya nzima ya Pangani pamoja na vijiji vyake vyote inapata nishati ya umeme ndani ya kipindi cha miaka miwili. 

Akielezea malengo ya kuipa kipaumbele wilaya ya Pangani kwenye mpango wa usambazaji wa umeme vijijini chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Profesa Muhongo alieleza kuwa ni kufuta umasikini kupitia uboreshaji wa huduma za jamii kama shule, zahanati, pamoja na kuzalisha ajira na kupunguza wimbi la vijana kukimbilia mjini kutafuta ajira. 

Alisema katika utekelezaji wa mradi wa REA Awamu ya tatu katika wilaya ya Pangani, maeneo yatakayopewa kipaumbele cha kwanza ni pamoja na shule, zahanati, vyuo, makanisani na misikitini. 

Aliwataka wananchi wa wilaya ya Pangani kujiandaa na mradi huo kwa kubuni fursa mbalimbali kama vile kuanzisha vikundi vidogo vidogo kwa ajili ya kuanzisha viwanda, ukulima na ufugaji wa kisasa ili kujipatia maendeleo. 

Alifafanua kuwa ni wakati wa wakinamama wa wilaya ya Pangani kuachana na matumizi ya kuni na kutumia majiko ya umeme na gesi. 

Profesa Muhongo aliendelea kusema kuwa miradi ya umeme haihitaji siasa na kuwataka wananchi kuweka nguvu zaidi kwenye uchumi kwa kutumia nishati ya umeme badala ya kupoteza muda kwenye siasa. 

Naye Mbunge wa Pangani Jumaa Hamidu Aweso (CCM) aliishukuru serikali kwa kuipa kipaumbele wilaya ya Pangani na kusisitiza kuwa wataanza kufanya uhamasishaji kwa wananchi wote wa Pangani . 

Aliwataka wananchi kuachana na maandamano ya siasa na badala yake waweke nguvu kwenye shughuli za kiuchumi zitakazowapatia maendeleo. 

Alisema kuwa mara baada ya umeme katika wilaya nzima ya Pangani kupatikana, wawekezaji watajitokeza kuwekeza kwenye viwanda vya korosho na kuongezeka mapato katika halmashauri ya Pangani.
Share on Google Plus

About Jestina George

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment