Upatikanaji wa huduma za afya na wahudumu wake umeongezeka tangu 2015 kutokana na ripoti za wananchi

10 Agosti 2016, Dar es Salaam: 

Utafiti wa Sauti za Wananchi wa Twaweza unaonyesha maoni chanya kutoka kwa wananchi juu ya sekta ya afya nchini Tanzania. Kwa mfano, ni asilimia 18 wananchi wanaoripoti kuona upungufu wa madaktari katika vituo vya afya miezi mitatu iliyopita, ukilinganisha na asilimia 43 walioliona tatizo hili mwaka 2015. Vilevile, asilimia 73 walisema waliheshimiwa ipasavyo mwaka 2016, idadi hii ikiongezeka kutoka asilimia 42 mwaka 2015. Usafi kwenye vituo vya afya ulionekana kuboreshwa mwaka 2016. Waliolalamikia jambo hili walipungua kutoka watu 3 kati ya 10 mwaka 2015, hadi mtu 1 tu kati ya watu 10 mwaka huu. Vilevile, malalamiko yahusuyo kushindwa kumudu gharama za matibabu pia yalipungua: mwaka 2015, asilimia 34 ya wananchi walisema gharama zilikuwa kubwa mno au hawakuweza kulipa gharama hizo huku mwaka 2016, asilimia 19 ndio waliolalamikia gharama hizo. Hata hivyo, upungufu mkubwa wa dawa na vifaa vingine muhimu vya afya bado ni tatizo sugu: mwaka 2015, asilimia 53 walisema hivyo ukilinganisha na asilimia 59 mwaka 2016.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kupitia muhtasari wa utafiti wake wenye kichwa cha habari cha Nyota njema huonekana asubuhi? Maoni ya wananchi kuhusu huduma za afya zinazotolewa na serikali ya awamu ya tano. Muhtasari huo unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Matokeo yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,836 kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara kati ya tarehe 2 na 17 Mei 2016 (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya).

Mwaka 2016, asilimia 61 ya Wananchi waliripoti kutibiwa katika vituo vya afya vya serikali. Hili lilikuwa ni ongezeko la mahudhurio ukilinganisha na asilimia 47 mwaka 2015. Kwa upande wa maduka ya dawa, wananchi waliotembelea maduka haya walipungua kutoka asilimia 19 mwaka 2015 hadi asilimia 13 mwaka 2016. Wale walioamua kutochukua hatua yoyote walipougua walipungua kutoka asilimia 8 mwaka 2015 hadi asilimia 2 mwaka 2016.

Asilimia 73 waliripoti kusubiri kwa muda usiozidi lisaa limoja kabla ya kumuona daktari. Wengi wao walikiri kupewa maelezo mazuri kuhusu maradhi yanayowasibu (asilimia 92) na kuandikiwa dawa stahiki (asilimia 81). Asilimia 70 walifanikiwa kupata angalau baadhi ya dawa walizozihitaji kutoka kwenye kituo hicho hicho cha afya.

Sambamba na suala la upungufu wa dawa na vifaa vingine muhimu, wananchi waliainisha changamoto zingine walizokumbana nazo katika vituo vya afya vya serikali kwa ujumla. Mojawapo ya changamoto hizo ilikuwa ukosefu wa vitanda (asilimia 31), mashuka (asilimia 27) na vyandarua (asilimia 29) vya kutosha kwa wale waliolazwa au waliomsindikiza mtu aliyelazwa. Pia, asilimia 36 waliripoti kuona mgonjwa zaidi ya mmoja akilala kwenye kitanda kimoja ukilinganisha na asilimia 30 mwaka 2015.

Sera inaeleza kuwa matibabu kwenye vituo vya afya vya serikali ni ya bure kwa wajawazito, watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wazee wenye miaka zaidi ya 60. Hata hivyo, wananchi wengi walisema walishawahi kushuhudia makundi haya wakitozwa gharama za matibabu: asilimia 41 ya wananchi walifahamu wazee waliolipia matibabu, asilimia 35 walifahamu walezi wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano walioambiwa walipie matibabu ya malaria ni asilimia 27 waliwajua wajawazito waliolipishwa matibabu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, ndugu Aidan Eyakuze, akitoa rai yake juu ya matokeo haya amesema “Takwimu hizi zinaonyesha mabadiliko chanya katika sekta ya afya. Pia, wahudumu wa afya wanapatikana muda mwingi zaidi na ni wasikivu pia. Vituo vya afya navyo ni visafi zaidi. Lakini upungufu wa dawa na vifaa vyingine, vikiwemo vitanda, mashuka na vyandarua bado ni changamoto. Katika siku za usoni itakuwa muhimu kufanya utafiti wa kina ili kuboresha huduma za afya na kuhakikisha kuwa wahudumu wa afya na vifaa vinapatikana. Kwanza, tutahitaji kutumia utafiti – wa kile ambacho kimefanikiwa, wapi na kwanini, na kile ambacho tunaweza kujifunza kutokana na mapungufu yetu. Pili, suala la motisha – kwa wale wote wanaohusika katika utoaji wa huduma za afya. Hapa itabidi tuanzie na wale walio mstari wa mbele, madaktari na wauguzi, hadi wale wanaoagiza dawa na kuzifikisha kwenye vituo. Pia motisha kwa wafanyakazi wa wizarani wanaotoa maamuzi ya kisera nayo itahitaji kuzingatiwa. Suala la tatu ni la ufuatiliaji – kuhakikisha kuwa tunafahamu nini kinachoendelea na kile wanachokutana nacho wananchi. Kwa sasa, dalili za maboresho zinafaa kusifiwa.
Share on Google Plus

About Jestina George

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment