WAPINZANI NCHINI ZAMBIA WATAKA WAPEWE NCHI.


Lusaka, Zambia. Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais wa Zambia yanaonyesha kuwa Rais Edgar Lungu anaongoza, huku wapinzani wakipinga matokeo hayo kwa madai kuwa hesabu zao zinaonyesha mgombea wao ndiye anayeongoza kama kura hazijachakachuliwa.

Lungu anakabiliwa na upinzani mkali wa Hakainde Hichilema, mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Muungano kwa ajili ya Maendeleo ya Taifa (UPND).

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ), Rais Lungu amepata kura 262,149 dhidi ya 243,794 alizopata mpinzani wake, Hichilema baada ya kura za majimbo 26 kati ya 156 kuhesabiwa.

Taarifa iliyotolewa na UPND imeeleza kuwa mfumo wao wa kuhesabu kura ulioenda sambamba na ule wa ECZ umeonyesha Hichilema amemshinda kwa kura za kutosha Lungu baada ya asilimia 80 ya kura zote kuhesabiwa.

Maofisa wa ECZ wamevionya vyama vya siasa kutoa taarifa za aina hiyo. Hata hivyo, vyama vyote vina uwezo wa kukusanya matokeo ya upigaji kura na kujumuisha kwa haraka kuliko tume hiyo.

Awali, ECZ ilitarajia kukamilisha kuhesabu kura jana katika uchaguzi huo ambao Wazambia waliwachagua pia wabunge, mameya na madiwani na kuamua juu ya mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba.

Hata hivyo, maofisa wa tume hiyo wamesema matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa baadaye bila ya kutaja siku na muda maalumu.
SOURCE: MWANANCHI
Share on Google Plus

About Jestina George

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment