WAZIRI MKUU AKAGUA KIWANDA CHA NGUO UBUNGO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza  baada ya kutembelea kiwanda cha kushona nguo cha Tooku kilichopo kwenye eneo la EPZ, Mabibo External jijini Dar es salaam Agost 10, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ushonaji wa suruali za Jeans wakati alipotembelea kiwanda cha kushona nguo cha Tooku kilichopo kwenye eneo la EPZ, Mabibo External jijini Dar es salaam  Agost 10, 2016 .  Kulia ni Balozi wa China nchini, Dkt Lu Youqing na kushoto ni Meneja Mkuu Msaidizi wa kiwanda hicho, Rigobert Massawe. 


*Aagiza Wizara ya Viwanda iendeleze eneo la Mkulazi, Morogoro

*Awapa kazi kazi maalum Wakuu wa Mikoa sita
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ihakikishe inaendeleza eneo la viwanda vya usindikaji mazao la Mkulazi lililopo Morogoro ili liwe kielelezo kikuu cha ukanda maalum wa kiuchumi (SEZ) unaoa mbaa sambamba na reli ya TAZARA.

Amesema wizara hiyo inapaswa ishirikiane kwa karibu na Mamlaka ya Uendelezaji Kanda Maalum za Kiuchumi (EPZA) pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Agosti 10, 2016) wakati akizungumza na watendaji wa EPZA na wafanyakazi wa kiwanda cha kushona nguo cha Tooku kilichopo eneo la Benjamin William Mkapa, Mabibo External jijini Dar es Salaam.

Pia amewataka wakuu wa mikoa sita ya Pwani, Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe kufanya kazi kwa karibu na EPZA kwa kuainisha maeneo yanayohitaji kuendelezwa kiuchumi ambayo yanafikika kwa urahisi kwa reli ya TAZARA.

“Wekeni mipango yenu kwa umakini ya kuanzishwa kwa kanda maalum za kiuchumi katika maeneo yenu ya kiutawala na mipango hii ijitokeze kwenye mipango ya maendeleo ya mikoa yenu, onyesheni mikakati ya uendelezaji viwanda inayoendana na Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa,” amesema.

Amewataka wakuu hao wa mikoa kuhakikisha wanaweka mfumo utakaoimarisha ulinzi wa miundombinu ya reli hiyo ili isiharibiwe na watu wenye nia mbaya.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amempongeza Balozi wa China hapa nchini, Dk. Lu Youqing kwa bidii aliyonayo ya kuleta wawekezaji hapa nchini. “Mwezi uliopita, nilienda Mlandizi kutembelea kiwanda cha nondo ambacho kinaendeshwa kwa ubia baina ya Tanzania na China. Pia nikaenda Mkuranga kwenye kiwanda cha kutengeneza marumaru (tiles), na leo hii tuna kiwanda cha Wachina ambacho kinashona nguo zinazopelekwa kuuzwa Marekani,” amesema.

“Nimefurahishwa kukuta asilimia 99 ya wafanyakazi humu ndani ni Watanzania, na asilimia moja iliyobakia ndiyo ya wageni na hawa wanafanya kazi za kitaalamu. Nimefurahi zaidi kukuta nguo zinazoshonwa na kiwanda hiki zimeandikwa MADE IN TANZANIA. Tena nimekutajeans za kisasa za Levis na Wrangler ambazo zinapendwa na vijana wengi na zilikuwa zikinunuliwa nje ya nchi, lakini hivi sasa zinazalishwa hapa nchini,” amesema.

“Hii ni ishara kuwa lengo la Mheshimwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli la kutaka Tanzania iwe nchi ya viwanda litatimia,” na kuongeza: “Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwa na viwanda ili tuuze mazao kama pamba, korosho, maharage ambayo yamesindikwa badala ya kuuza mazao ghafi”.

Amesema amepewa taarifa kwamba kiwanda hicho kimekwishaajiri wafanyakazi 1,500 na kitaendelea kuajiri hadi wafikie zadi ya 6,000 waaohitajika. Amewataka vijana walioajiriwa kufanya kazi kwa bidii.
Mapema, akimtembeza Waziri Mkuu kwenye kiwanda hicho, Meneja Mkuu Msaidizi wa kiwanda hicho, Bw. Rigobert Massawe alisema wafanyakazi hao wanafanya kazi kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 11 jioni wakiwa na saa moja ya mapumziko ya mlo wa mchana halafu wanarudi tena saa 12 jioni hadi saa 1 usiku ikiwa ni masaa ya ziada (overtime).

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Kanali (Mst). Joseph Simbakalia alisema mamlaka hiyo ilianzishwa ili kuanzisha, kuendeleza na kusimamia uanzishaji na urejeshaji wa viwanda hapa nchini.

Akitoa taarifa kuhusu mamlaka hiyo Waziri Mkuu, alisema mamlaka hiyo ilianza na mtaji wa dola za marekani milioni 22 lakini hivi imefikisha dola za marekani bilioni 4 kutina na makampuni 140 ambayo yamewekeza hapa nchini.

Kuhusu kiwanda cha kushona nguo cha Tooku, Kanali Simbakalia alisema kabla ya kuajiri, kiwanda hicho kinatoa mafunzo kwa vijana 400 ambao wanafanyiwa usaili kila baada ya miezi mitatu na wataendelea kufanya hivyo kwa makundi 10 -12 hadi wafikishe idadi ya wafanyakazi 6,000 wanaotakiwa.

Alipoulizwa na Waziri Mkuu wanatumia utaratibu gani kuwapata vijana hao, Simbakalia alisema utaratibu unaotumika ni kutuma barua ya maombi, nakala ya cheti cha kuzaliwa na barua ya mtendaji kutoka kwenye Serikali za Mitaa eneo analoishi muombaji. Alisema sifa kubwa ni kujua kusoma na kuandika.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
JUMATANO, AGOSTI 10, 2016

Share on Google Plus

About Jestina George

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment