‘Scorpion’ uso kwa uso na anayedai kumtoboa macho


 December 14 2016 Kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi inayomkabili Salum Njwete ‘Scorpion’ imeendelea katika mahakama ya wilaya ya Ilala wakati shauri hilo lilipoletwa kwa ajili ya kusikilizwa.
Kesi hiyo ina mashahidi sita na mpaka sasa ameshasikilizwa mmoja ambaye ni shahidi namba moja Said Mrisho ‘aliyetobolewa macho’ ambaye ametoa ushahidi wake mahakamani hapo akielezea tukio alilofanyiwa.
Baada ya kusikiliza kesi, mahakama hiyo imeahirisha shauri hilo hadi December 28 mwaka huu ambapo itaendelea na shahidi wa pili.
Mrisho, ambaye ndiye shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, aliieleza mahakama hiyo kuwa alichomwa visu tumboni na mgongoni kabla ya kutobolewa macho.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule, Mrisho alidai kuwa wakati tukio hilo linaendelea, alimkariri mshitakiwa kwa kumuangalia usoni.
Akielezea tukio lilivyotokea, alidai Septemba 6, mwaka huu saa nne usiku alikuwa kazini kwake Tabata Segerea kwa kazi yake ya kinyozi na baada ya kufunga ofisi, alikwenda kituoni kusubiri usafiri wa kwenda nyumbani kwake Makuburi, karibu na Ubungo.
Alidai wakati anasubiri usafiri, ilipita bajaji na kumuuliza anakokwenda, ambapo alimwambia kwamba anakwenda Ubungo na mwenye bajaji alidai anakwenda Buguruni, ila anaweza kumsogeza hadi Tabata Relini ili akapande magari ya Ubungo.
“Wakati nishapanda bajaji na tumeelewana anifikishe Tabata Relini ghafla dereva huyo aliniomba apite njia ambayo ni fupi kutokezea Buguruni, ambapo hapo ndiko nitakapochukulia magari ya Ubungo kwani naishi Makuburi,” alidai Mrisho.
Alidai baada ya kufikishwa Buguruni Kwa Mnyamani, aliona wauza kuku na kusogea kwa ajili ya kununua ili kupeleka nyumbani kwake.
“Kulikuwa kuna wafanyabiashara wengi wa kuku eneo la Buguruni kituo kinaitwa Kwa Mnyamani kama saa 4:40 usiku ambapo nilinunua kuku mmoja kwa Shilingi 6, 000,” alidai.
Akiendelea kutoa ushahidi, Mrisho alidai wakati anaendelea na manunuzi na kuongea na muuzaji, aliona mtu amesimama upande wake wa kulia na alianza kumuita.
“Aliniambia ‘broo’ nina shida. Nami nilimgeukia na kumuuliza una shida gani kama una shida sema nakusikiliza kama naweza kukusaidia nikusaidie, lakini mtu huyo hakujibu ambapo niliendelea na manunuzi,” alidai.
Shahidi alidai wakati anaendelea na manunuzi alishikwa na hofu, kwani mkono wake alikuwa amevaa cheni ya silva na mfuko wa suruali, ulikuwa na fedha iliyokuwa inaonesha kutuna.
“Ghafla nilishtukia ninachomwa visu mkononi na bega la kushoto ambapo nilipogeuka niliendelea kuchomwa na nikaanza kupiga kelele ya mwizi lakini sikupata msaada, kwani nilishangazwa kuona watu wananiona lakini hawanipi msaada,” alidai na kuongeza, “Yule mtu alijibu hakuna mtu wa kumsaidia ambapo aliendelea kumchoma visu vinne tumboni na kuanguka chini wakati huo kuna watu walikuwa wanamwita Scorpion, kwamba tayari umeshaua huku akiendelea kunikagua mfukoni,” alidai.
Alidai wakati anaendelea kukaguliwa, mshitakiwa alimkanyaga mkono wake na kumkata cheni ambayo alikuwa amevaa mkononi na shingoni. Pia, alidai kuwa alivyodondoka chini alidondoka chali kwa hiyo alikuwa na nafasi ya kumkariri vizuri jinsi alivyo, kwa kuwa kulikuwa na mwanga wa taa.
Aliiambia mahakama kuwa, mshitakiwa aliendelea kumkagua mfukoni na kuchukua fedha zote na kwamba alisikia sauti kuwa, “Salum mwache huyo keshakufa sasa ukimchukulia na simu ndugu zake watajulishwaje?” Shahidi alidai baadaye alivuliwa fulana na kumfunga mkononi kisha akamburuza kumpeleka barabarani huku akiwaambia wenye magari wamgonge.
“Muda huo nilikuwa sijatobolewa macho ambapo niliwekwa barabarani ili nigongwe na gari, lakini yalikuwa yananipita nilikaa barabarani kama nusu saa wakati huo yeye kasimama pembeni. “Baada ya muda alinivuta pembeni na kunipiga kisu cha jicho la kushoto ambapo nilipoteza fahamu kwa muda na baadaye nilisikia mtu anadai yeye ni raia mwema anataka kunisaidia ambapo nilimpa simu na kuanza kuwasiliana na ndugu zangu,” alidai.
Shahidi huyo alidai baada ya muda alisikia gari la polisi limefika na kumchukua hadi kituoni kwa ajili ya kupewa Fomu Namba Tatu(PF3) kwa ajili ya matibabu. Aidha, alidai kwa kuwa alikuwa anasikia maumivu, alichukuliwa maelezo akiwa ndani ya gari ambapo baadaye alifikishwa Hospitali ya Amana na kupewa huduma ya kwanza.
Shahidi huyo alidai alipofika Amana, alikutana na ndugu zake na baada ya muda alipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo alipewa kitabu cha kusaini kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji tumboni. Pia alidai baada ya muda, daktari wa macho alimfanyia uchunguzi na kueleza kuwa macho yametobolewa, ambapo alikaa hospitali kwa siku sita.
Kabla ya kuanza kutoa ushahidi huo, mshitakiwa ambaye alipandishwa kizimbani saa 3.35 asubuhi, aliomba mahakama isianze kusikiliza shauri hilo hadi wakili wake wa utetezi afike. Mahakama hiyo ilikubaliana na ombi hilo, ambapo baada ya dakika 15 kupita wakili alifika na kuanza na usikilizwaji.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa ambaye ni mwalimu wa karate, alitenda kosa hilo Septemba 6, mwaka huu maeneo ya Buguruni Sheli wilayani Ilala.
Ilidaiwa mshitakiwa aliiba cheni ya dhahabu gramu 38 yenye thamani Shilingi 60,000, kibangili cha mkononi na Sh. 331,000 pamoja na pochi, vyote vina thamani ya Sh 476,000, mali ya Said Mrisho.
Ilidaiwa kabla ya wizi huo, alimchoma na kisu tumboni mgongoni na machoni. Kesi hiyo itaendelea na ushahidi Desemba 28, mwaka huu na mshitakiwa alirudishwa rumande.
Share on Google Plus

About mwanaidinuhu

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment

Note: only a member of this blog may post a comment.