LHRC yasisitiza kuwepo usawa wa kijinsia katika uteuzi unaofanywa na Rais Magufuli

Hii ni taarifa ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kuhusu mwenendo wa masuala ya kijinsia katika teuzi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika nafasi mbalimbali za uongozi nchini Tanzania.


Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimetathmini mwenendo wa masuala ya kijinsia katika teuzi mbali mbali zinazofanywa na Serikali katika nafasi mbalimbali za uongozi nchini Tanzania. Katika tathmini yetu tumejikita zaidi kuangalia katika muktadha wa Haki za Binadamu na haki za Wanawake kwa kuzingatia mikataba mbalimbali ya kimataifa na Kikanda ambayo Tanzania imeridhia kuhusu usawa wa kijinsia vile vile kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano w Tanzania ya mwaka 1977 na pia sheria nyinginezo.
Tukianza na kikanda, Tanzania ni nchi mwanachama wa Umoja wa nchi za kusini mwa Afika na hivyo imeridhia mkataba wa Jinsia na Maendeleo wa nchi za Kusini mwa Afrika yaani SADC Gender Protocol ambapo mkataba huu katika Ibara ya 12 inazitaka nchi wanachama kuhakikisha kuwa katika ngazi zote za maamuzi kuna usawa wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50. Pia Mkataba wa Afrika wa Haki za Wanawake (Maputo Protocol) unapinga ubaguzi dhidi ya wanawake katika ngazi za maamuzi.
Kimataifa, Mkataba wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW) Katika Ibara ya 7 inazitaka nchi wanachama wa mkataba huo kuhakikisha wanawake wanashirki kikamilifu katika kutunga sera, sheria na kuwa katika ngazi za utekelezaji wa sera na sheria hizo (ngazi za maamuzi).
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 13 inaeleza jinsi ambavyo serikali itachukua hatua za makusudi kurekebisha matatizo yaliyo katika jamii ili kuondoa ubaguzi. Katika jamii kuna mfumo dume na mifumo mingine kandamizi ambayo imesababisha wanawake wengi kukosa fursa ya kusoma, kuwa na kipato kidogo, kutopata nafasi ya kuwa viongozi na kadhalika. Hii imepelekea wanawake wengi kushindwa kugombea na kuwa wachache katika ngazi za maamuzi. Ndio maana jitihada mbalimbali za makusudi zinapaswa kufanyika ili kuweka nafasi maalum kwa ajili ya kurekebisha tatizo hilo katika jamii.
Katika muktadha huo Katiba ya Jamhuri ya Muungano imetoa mwongozo katika teuzi mbalimbali, kwa mfano Wabunge wateule wa Rais. Ibara ya 66 (1) (e) inasema na tunanukuu:
‘… Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya ibara hii, kutakuwa na aina zifuatazo za Wabunge, yaani:-…(e) Wabunge wasiozidi kumi walioteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizotajwa katika aya za (a) na (c) za ibara ya 67 na angalau wabunge watano kati yao wakiwa wanawake…”
Ibara hiyo ya katiba inamaanisha kuwa katika kuteua wabunge wa kuteuliwa na Rais anapaswa kuhakikisha idadi ya wanawake haipungui watano; Neno angalau maana yake sio chini ya.
Katika kufanya tathmini ya wabunge walioteuliwa na Rais, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimebaini kuwa mpaka sasa Rais ameshateua wabunge kama ifuatavyo:
1. Mhe. Dr. Tulia Ackson (KE)
2. Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (KE)
3. Mhe. Dr. Abdalla Possi (ME)
4. Mhe. Dr. Augustine Philip Mahiga (ME)
5. Mhe. Dr. Phillip Isdor Mpango (ME)
6. Mhe.Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (ME)
7. Mhe.Prof. Abdallah B ulembo (ME)
8. Prof. Palamagamba Kabudi (ME)

Katika hao watajwa hapo juu idadi ya wanaume tayari wako sita, ambapo ukwelihuu unakinzana na ibara ya 66(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata Rais akichagua wanawake tu katika nafasi zilizobakia, bado haitakidhi haja ya kuwa na wanawake watano au zaidi kwa mujibu wa Katiba.
Pia tumeangalia katika nyadhifa zingine za uteuzi unaofanywa na Rais kama Mawaziri na Manaibu waziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, wakurugenzi wa Halmashauri bado idadi ya wanawake imekuwa chini sana na hivyo kutokuzingatia ulinganifu wa kijinsia. Kwa mfano idadi ya mawaziri wanawake ni 4 tu kati ya 19, kati ya wakuu wa mikoa 26 wanne tu ndio wanawake, kati ya wakuu wa Wilaya 134 wanawake ni 25 tu na kati ya wakurugenzi wa halmashauri na Wilaya 185 wanawake ni 33 tu.
Kutokana na hali hiyo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaitaka Serikali na mamlaka nyingine za uteuzi;
i) Kuzingatia Sheria na Katiba katika teuzi mbalimbali katika nafasi za uongozi.

ii) Kufuata misingi ya Haki za Kijinsia kwa mujibu wa mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo Serikali imesaini na kuridhia.
iii) Kuzingatia usawa wa kijinsia na kuchukua hatua za maksudi (affirmative action) ili kuwa na jamii yenye haki na usawa katika suala la uongozi wa nchi.
iv) Rais aone uwezekano wakurekebisha hii hali iliojitokeza ya kukiuka maelekezo ya katiba
Imetolewa leo tarehe 19 Januari 2017 na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.
Share on Google Plus

About mwanaidinuhu

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment