Wamiliki wa runinga wataka wananchi walipie huduma ya matangazo

Warusha matangazo ya televisheni na wenye vituo vya utangazaji wamependekeza matangazo ya bure yaondolewe na badala yake wananchi walipie.

Mapendekezo hayo yametolewa kwenye mkutano wa kukusanya maoni ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa lengo la kuja na marekebisho ya gharama za kurusha matangazo ya televisheni ambayo huumiza pande zote.
Akichangia, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Agape Associates Limited wenye king’amuzi cha TING, Andy Fernandes alipendekeza vituo vya utangazaji viwalipe warusha matangazo (wenye ving’amuzi) dola za Marekani 2,500 (zaidi ya Sh milioni tano) kwa mwezi huku akisisitiza pia mlaji wa mwisho (mwananchi) alipie kiasi matangazo hayo.
“Wakati umefika sasa kwa mlaji wa mwisho (mwananchi) kulipa gharama za kuangalia matangazo ambazo zitamsaidia kumpunguzia makali mwenye kituo cha utangazaji, hata hospitali watu wanachangia,” alisema kauli iliyoungwa mkono na Kampuni za Star Media (T) Limited na Basic Transmission Limited ambao walipendekeza mwananchi alipie Sh 6,000 kwa mwezi.
Kwa upande wa vituo vya utangazaji, wao wamependekeza kuwepo na nafasi ya kufanya biashara kati yao na warusha matangazo, wapate fursa ya kuuza vipindi.
Edward Komba wa Abood Media alisema: “Vituo vilivyo mikoani vimekuwa na gharama kubwa ya kuandaa vipindi huku kukiwa na ugumu wa upatikanaji wa matangazo na kupendekeza vituo vilipe shilingi laki sita kwa warusha matangazo kwa mwezi.”
Sylvia Mushi wa Capital Television alipendekeza warusha matangazo wanunue vipindi kutoka kwenye vituo vya utangazaji na wao kupata fedha za kujiendesha kwa kumtoza mwananchi.
Hata hivyo, baadhi ya vituo vya televisheni vinavyotoa elimu au vya dini kama vile Mlimani TV, SUA ambao wamependekeza kuwapo na kundi maalumu la vituo ambavyo havitalipia gharama hizo kutokana wao kutoa huduma zaidi na si biashara.
Naye Mary Msuya wa Baraza la Wateja wa Huduma za Mawasiliano la TCRA, alisema pamoja na hoja za wadau za kuwa gharama za utangazaji kuwa juu, alitaka wananchi wa kawaida waendelee kupata matangazo bure husani kwa vituo vitano vyenye leseni ya kitaifa.
Awali, Mwenyekiti wa Jopo la Uchunguzi la TCRA, Jaji mstaafu Eusebia Munuo alisema kabla ya kuwasikiliza wadau wa utangazaji, umefanyika utafiti wa kuangalia gharama za urushaji wa vipindi vya televisheni kwa kuangalia gharama zenye ufanisi, zinazotambulika na zisizoumiza upande wowote.
“Tulishapata maoni tulipotembelea kampuni yanatorusha matangazo (wenye ving’amuzi) na hata vituo vya utangazaji baadhi waliotoa maoni yao kimaandishi, lakini leo tumetoa nafasi ya kusikiliza maoni zaidi,” alisema Jaji Munuo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Utangazaji wa TCRA, Andrew Kisaka alisema lengo ni kuhakikisha pande hizo mbili zinatoa mapendekezo ya ada ya kurusha vipindi huku mwananchi akipata matangazo moja kwa moja bila kulipia
Share on Google Plus

About mwanaidinuhu

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment