TCRA yakanusha kurekodi mazungumzo ya watumiaji wa simu

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewaonya watumiaji wa huduma za mawasiliano kuacha kutoa taarifa zinazowapa taharuki wananchi kuwa mamlaka hiyo imeanza kurekodi mazungumzo ya kwenye simu.

Akizungumzia ujumbe ambao unasambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakyanjala alisema ni kosa la jinai kwa mtu kueneza taarifa za uzushi zenye lengo la kuibua taharuki miongoni mwa jamii.
Mwakyanjala alisema si kweli kuwa mazungumzo ya simu yanarekodiwa na TCRA, kwani kwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na haki ya mtumiaji wa huduma za mawasiliano.
“Mawasiliano ya simu ni masuala ya siri kati ya wahusika, sheria hairuhusu kusikiliza wala kurekodi mazungumzo, hata kama kampuni za simu zitatoa taarifa za wateja wao kwa mtu mwingine tunazichukulia hatua.
“Kama kuna suala la uvunjifu wa amani ambalo linatakiwa kufuatiliwa, basi kuna vyombo vya usalama ambavyo ndio pekee vinaruhusiwa kupewa taarifa hizo na si vinginevyo,” alieleza ofisa huyo wa TCRA.
Mwakyanjala alisisitiza kuwa maofisa wa TCRA wanafanya kazi kwenye ofisi za mamlaka hayo na si kwenye maduka au minada, na kuwa kama kuna mabadiliko au taarifa zozote, basi zitatolewa na ofisi husika itatoa taarifa.
Tangu juzi kumekuwa na ujumbe ambao umekuwa ukitumwa kwenye mtandao wa WhatsApp ikimnukuu mtu anayedai kukutana na ofisa wa TCRA wakiwa dukani na alimwambia kuanzia sasa simu zote zitarekodiwa hivyo wajihadhari na kuzungumza mambo ya uzushi ya watu wa serikalini au mambo yanayohusu siasa.
Ujumbe huo pia umezidi kueleza kuwa ili kujua simu inarekodiwa basi utasikia milio tofauti tofauti kabla ya simu kuanza kuita.
Share on Google Plus

About mwanaidinuhu

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment