Tuziangalie faida na hasara za kuanikwa kwa mastaa wanaohusishwa na dawa za kulevya

Nianze kwa kusema madawa ya kulevya yameharibu sana vijana wa nchi hii, vijana ambao ni nguzo kubwa ya taifa hili. Naiunga mkono serikali ya awamu ya tano katika kupigana vita hii ambayo sio ndogo kwa kweli kwa maana wahusika wapo gizani ni watu wanaojificha na kuifanya biashara hii kiumakini mno ili wasitiwe nguvuni, na kuwa kwao gizani kunasababisha mamlaka husika zifanye kazi usiku na mchana.


Serikali yetu kama serikali zingine imeshakamata watu wengi na madawa haya, wengine wameshafungwa na wengine kesi zao zinaendelea wakiwa ndani. Wengine walikiri mbele za mahakama kuwa ni wabebaji au ni wauzaji na wakafungwa kwa mujibu wa sheria.
Hapa majuzi mpaka sasa nchini kuna mijadala katika vijiwe na mitandao ya kijamii na sehemu mbalimbali kuhusu suala hili la madawa ya kulevya. Mijadala hii imeegemea zaidi katika style inayotumika katika vita hii ya madawa ya kulevya. Kuna makundi yanayodai style iliotumika sio sahihi na makundi mengine yanadai ni sahihi. Kuna makundi yanadai kundi linalokamatwa sio hasa linalotakiwa.
Kwa kifupi katika makala yangu sitaki kujiweka katika kundi lolote ila nikiwa mwananchi mwenye uhuru wakuelezea mawazo yangu naomba nielezee ili tuchangiane mawazo. Mimi baada ya kuona watu maarufu(nimetumia neno hilo la maarufu kwakuwa watu hao wanatoka kwenye tasnia tofauti kwa hiyo nimejumuisha)kuitwa polisi kupigwa picha na waandishi wa habari na kuwekwa ndani, nikaanza kujiuliza maswali mengi sana, ila swali kubwa na la msingi lililotawala kichwani mwangu ni je, kwa kukamatwa kwao kuna faida kiasi gani na hasara kiasi gani?
Mimi naamini mkuu wa mkoa na watu wa usalama walilijadili suala hili mpaka kufikia uamuzi huo, ila najiuliza kwanini mamlaka hizo hazijawahoji wasanii hao kimya kimya? Kwa nini wasingewasiliana na wizara husika ambayo wasanii hao wapo chini yake? Maana naamini Kamera hazitosaidia chochote katika mahojiano hayo, kama wao niwauzaji au watumiaji kuwapiga picha haitosaidia zaidi itafanya wahusika wengine wawe na habari ya kinachoendelea na kujidhatiti hasa msumeno utakapowafikia au hata kutoroka.
Mimi sitetei wasanii wavute madawa au wabebe au wauze hapana, ila tukumbuke hawa ni wasanii ambao wanatumia nguvu kubwa sana kufika walipofika bila sapoti ya aina yeyote kutoka popote, wasanii ambao wanafanya kazi zao bila ngazi ya kuwasaidia wapande juu, mamlaka zilizopo za kuwapa sapoti wasanii kurahisisha kazi hizo mamlaka hizo zipo kama hazipo. Hata basi kama hamuwapi sapoti basi wapate heshima, wasanii wanarukishwa kichura chura hii ni dhahiri hawaheshimiwi na napata picha kwa style hii tasnia za muziki na filamu zitambuwe wao ni yatima.
Nataka watu watambue balozi zilizopo hapa nchini hazipo kwa ajili ya ushirikiano kiuchumi tu, zipo hapa katika kila nyanja ya mahusiano baina ya nchi husika. Balozi hizi hupeleka taarifa kila siku katika nchi zao. Nataka watu watambue pia jinsi ambavyo Tanzania ina waandishi wake nchi mbalimbali duniani ili kupata habari za kimataifa pia hizo nchi zina waandishi wake hapa Tanzania ili kupeleka kwao habari za kimataifa, kwahiyo tusishangae siku wasanii wetu wakinyimwa visa kwenda katika nchi za watu, au wakapata visa ila wakifika katika airports zao wakasachiwa masaa hata matano na nguo wakavuliwa zote maana sie wenyewe hatuwathamini.
Hawa wasanii hasa wa muziki ndio kama kitu kinachoipaisha juu nchi yetu kwa sasa baada ya tasnia mbalimbali kufeli. Sapoti ni muhimu sana kwa hawa watu na sio kuwarudisha nyuma, ndio mana nasema ingetumika njia nyingine hata ya kisiri kuwahoji.Turudi pale pale faida na hasara ya walichofanyiwa zipimwe ili tujue kwa kilichofanyika faida ni kubwa kuliko hasara au hasara ni kubwa kuliko faida?
Vijana wetu wa muziki wamefikia hatua ya kufanya muziki na wanamuziki wakubwa Afrika na hata Marekani ambako ni nchi iliyofanikiwa zaidi katika tasnia hiyo. Hata sasa hivi kuna wimbo unaopigwa sana kila sehemu wa mwanamuziki mkubwa wa hapa kwetu akiwa amemshirikisha mwingine mkubwa wa Marekani. Ndio nchi inatangazwa hivyo. Ila tusishangae mameneja wa wanamuziki wa nje kukataa kushirikiana tena na wanamuziki watanzania maana watawachafua wasanii wao pia.
Majuzi mwanamuziki wa hapa Tanzania alipata mualiko kwenda kutumbuiza kwenye ufunguzi wa fainali za AFCON Libreville nchini Gabon, tuliona akikabidhiwa bendera na kiongozi ikiwa ina maana akatangaze nchi na kweli alitangaza, ila kwa utaratibu huu itakuja kuwa ngumu kuja kuitwa kwenye hafla hizo. Msanii huyo majuzi juzi kanunua nyumba nchini Afrika Kusini ila tusishangae tukisikia kafukuzwa au haruhusiwi mwingine kununua nyumba nchini humo au kwingineko tusishangae maaa dunia inatazama.
Kale kamsemo ka dunia kijiji sio kamasihara ni kweli dunia ni kijiji kila mambo tunayoyafanya tusiyaangalia kitaifa tena bali kimataifa. Dunia ni kijiji kweli kweli ,zamani mtu aliye karibu na tukio ndio wa kwanza kupata habari, sasa hivi ni tofauti kabisa ni aliye karibu na kompyuta,simu ya smart n.k ndio mtu wa kwanza kupata habari, wingi wa kilomita sio suala tena. Turudi kule tena, e kwa tukio lililofanyika hasara ni kubwa au faida ndio kubwa?
Hapa Tanzania kuna waandishi wengi wa habari wa kutoka nje ya nchi kama nilivyosema, na vyombo vikubwa vya habari vya dunia vipo hapa, kukamatwa kwa watu katika suala lolote hua ni habari lakini siku wakikutwa hawana hatia wakaachiwa huwa sio habari tena. Habari za kujua hawana hatia watakaojua ni wachache, watakuwa walishachafuka na ole wao hata mwakani mmoja wa wasanii hao akanunua gari la gharama kubwa kwa hela ya halali, kitu cha kwanza kitakachofika vichwani mwa watu ni tukio hili la wiki hizi. Turudi kuleee kuwakamata wasanii tena kwa mapicha ni kipi kinazidi kingine kati ya hasara na faida?
Tuige kwa walio juu yetu, Marekani ina vitengo rasmi vinavyojishughulisha na upingaji wa biashara ya madawa ya kulevya, kuna DRUGS ENFORCEMENT ADMINISTRATION (D.E.A), kuna FEDERAL BUREAU OF INVESTIGATION (F.B.I), kuna IMMIGRATION AND CUSTOMS ENFORCEMENT(I.C.E) na US BORDER PATROL. Hawa wote wanashirikiana kwa karibu mno.
Uingereza kuna THE SERIOUS ORGANISED CRIME AGENCY (SOCA), kuna NATIONAL CRIMINAL INTELLIGENGE SERVICE(NCIS).
Tanzania napo tunacho kitengo maalumu cha anti drugs na kitengo hicho kina wafanyakazi wengi tu na wa kutosha, wanapokamatwa akina TID ili waoneshe big fish ni akina nani? Je hawa anti drugs wanakuwa wanaenda kufanya nini kazini asubuhi mpaka jioni? Anti drugs wanalipwa mishahara kila mwezi ili watoe majibu ya maswali ambayo leo hii anaulizwa Wema.
Magereza yetu yamejaa wafungwa ambao wameshakutwa na hatia kwa kukutwa na madawa mengi sana kwenye matumbo yao au mabegi yao, wamekutwa na madawa hayo majumbani kwao,airports na mipakani, na baadhi yao walikubali mashtaka hayo, je habari nzuri ya wauzaji wakubwa unaipata kwa mtu anayevuta kete moja au kwa mtu aliyekamatwa airport na kilo mbili tumboni? Turudi kuleee kuwakamata wasanii na kuwapiga mapicha kuna faida zaidi au hasara zaidi?
Kama D.E.A ya USA ingekwenda kumkamata mwanamuziki DMX ili awaoneshe wapi ananunua madawa au kama anauza na kumpiga mapicha, nadhani serikali ya Marekani isingetumia tena trilioni nne(4) za kitanzania kwa mwaka kuendesha D.E.A,maana ingeonekana hakuna intelijensia kwahiyo kwa nini hela zote hizo zitumike, intelijensia ni muhimu katika mambo kama haya kwa hiyo kama wapo wanaolipwa kufanya kazi hiyo basi waifanye.
Serikali na wananchi tuwaheshimu hawa vijana wanaojitafutia riziki zao na kuwaajiri wenzao kwa njia ya sanaa, wasanii hawa wapo ambao wameajiri wenzao moja kwa moja na watu wanaendesha familia zao, mapromota mikoani wanaendesha familia zao kwa kupitia hawa hawa wasanii, serikali nayo inaingiza kipato sasa hivi kupitia hawa hawa wasanii, kuna wasanii wameajiri zaidi ya watu 20, ajira zenyewe hakuna siku hizi,wanaojiajiri tuwaheshimu na kuwasapoti na kama hatuwasapoti angalau tuwaheshim. Leo hii kwenye instagram kuna dada maarufu wa Kenya kaandika kuwa kila mtu maarufu Tanzania anauza madawa kiasi kwamba hewa yenyewe ya Tanzania imejaa madawa na kila mtu Tanzania kalewa.
Hapa nchini kwetu kuna msemo kinga ni bora kuliko tiba, kwakuwa hapa Tanzania hakuna hata shamba moja la kuzalisha “unga” basi dhahiri yanaingizwa ndani ya mipaka yetu, tukio walilofanyiwa wasanii walitakiwa wafanyiwe waliopewa mamlaka ya kuzuia madawa hayo yasiingie nchini. Kukamata wavutaji au wabebaji ambao wapo ndani ya nchi tena bila madawa hiyo ni tiba kinga ni kuweka vita hii kwenye mipaka yetu yote na viwanja vyetu vya ndege.
Siku zote mvutaji husaidiwa, mbebaji na muuzaji hukamatwa na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria.
Wasanii wetu kama wanahusika na uuzaji wa madawa ya kulevya basi sheria ni msumeno washughulikiwe ila sio kwa njia ya matangazo au kukomoana maana dunia inatazama, ila kama kuna njia nyingine ya kuwapata tuaowataka basi itumike hiyo, kwani narudi kulee njia ilioyotumika kipi ni zaidi kati ya faida na hasara?

Mungu ibariki afrika mungu ibariki Tanzania

Makala imeandikwa na Paul Sekaboyi
Share on Google Plus

About mwanaidinuhu

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment