Roma kaumia na anateseka, sahau blah blah za mtandaoni


Ni kama naota kwa hiki nachokisikia na kinachendelea mitandaoni kwa sasa. Siku chache zimepita tuliona ujumbe ulienea katika mitandao ya kijamii ukisomeka “WAKO WAPI WAKINA ROMA?” huku vilio na dua nyingi kutoka kwa mashabiki, wadau, viongozi wa dini na wa kisiasa pamoja na watu wengine walikuwa wakiwaomba zikisikika.

Mungu ni mwema na huwa hachoki kumpa na kumjibu yule amuombaye. Hatimaye Jumamosi asubuhi kupitia mitandao hiyo hiyo zilienea taarifa za kupatikana kwa Roma Mkatoliki, Moni Centralzone, Bin Laden na Imma ambao walitekwa usiku wa Jumatano ya wiki iliyopita na kupelekwa sehemu isiyojulikana.
Baada ya huzuni kugeuka furaha kwa siku moja hatimaye sasa furaha hiyo imegeuka kuwa matusi na kejeli kutoka kwa baadhi ya watu maarufu na wengine ambao wanadai tukio hilo halina ukweli wowote na kulifananisha na kiki kwa watu hao waliotekwa.
Baadhi ya redio mbao zinadai kuwa Roma na wenzake waliotekwa walilipwa kiasi cha dola 5000 kuikamilisha filamu hiyo. Lakini kwa hili nililoliona jana kwa Roma na wenzake waliotekwa, zaidi kwa Roma ambaye ni rapper mpambanaji kutokana na majeraha aliyonayo imewainamisha kwa sura za aibu wale wote waliokuwa mstari wa mbele katika kusambaza ‘upuuzi’ huo ambao ndani yake haukuwa na utafiti wa kutosha tena mbaya zaidi ni watu maarufu ndio wameonekana kufanya kitu hicho.

Fikiri kabla ya kutenda, unatakiwa kujiuliza kutokana na kile kilichoonekana kwa Roma, je thamani ya dola 5000 ambazo wanadai kulilipwa kwa ajili ya kutengeneza hiyo sinema inalingana na zile alama za damu zilizoonekana kwenye mwili wake ambapo imetenganisha rangi ya ngozi ya mwili wake na alama alizozipata? Na lile jino Je? Vipi kuhusu mguu wake na mkono wake wa kushoto?
Ukimuona mtu mzima analia ujue kuna jambo, nimemshuhudia Roma akikohoa kwa shida huku akikutana na maumivu makali anayoyapata. Sauti ya Roma inashindwa kusikika kama vile tulivyomzoea, hata kuongea muda mrefu hawezi kutokana na maumivu anayoyapata kutokana na mateso ambayo wameyapata huko walikopelekwa.
Tusiwafanye wenzetu waliopatwa na majanga hayo kuzidi kuwaweka katika wakati mgumu wakati tayari wametoka katika chupa ndogo iliyofungwa na mfuniko ambapo walikaa humo kwa siku tatu huku wakipata mateso, hakika hakuna anayeweza kuvumilia hilo.
Hakuna anayeijua kesho yake, “Usimtukane mamba kabla haujavuka mto” angalia lisije likakutokea wewe ukashindwa wa kumtazama wala kuzungumza naye kutokana na maneno yanayokufanya yakutoke kwa ajili ya kufurahisha baraza la mitandaoni huku ukiuweka utu pembeni.
Napenda kutanguliza pole kwa Roma, Moni, Imma na Bin Laden ambao wamepatwa na mkasa huo.
Share on Google Plus

About mwanaidinuhu

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment