Namuachia Mungu

Matukio ya kihalifu na mauaji yanayofanywa na watu wasiofahamika, yameendelea kutokea wilayani Kibiti baada ya viongozi wawili wa Kijiji cha Mangwi, Kata ya Mchukwi kuuawa kwa kupigwa kwa risasi, huku Mbunge wa Jimbo la Kibiti akisema anamuchia Mwenyezi Mungu kutokana na mauaji hayo.

Viongozi waliouawa usiku wa kuamkia jana ni Hamis Mkima ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mangwi na Mtendaji wa kijiji hicho, Shamte Rashid. Alipoulizwa kuhusu mauaji yanayoendelea Kibiti, Mbunge wa Jimbo la Kibiti, Ally Ungando (CCM), hakuwa tayari kuzungumzia kwa kina matukio ya kihalifu na mauaji yanayotokea zaidi ya kusema, “Sina cha kuzungumza, namuachia Mungu.”
Tangu kuanza kwa mfululizo wa mauaji ya polisi na raia katika maeneo hayo, zaidi ya watu 35 wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakiwamo polisi 13. Akizungumza na gazeti hili jana, Mtendaji wa Kata ya Mchukwi, Ami Ali aliwataja waliouawa ni Mkima ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mangwi na Mtendaji wake, Rashid.
Ali alisema siku hiyo ya tukio, watu wenye silaha walienda nyumbani kwa mwenyekiti wakamteka na wakamlazimisha awapeleke kwa viongozi wengine wa kijiji hicho. “Walipomteka, inasemekana mwenyekiti alijaribu kuwatoroka ndipo walimpompiga risasi ya mguu na kuondoka naye hadi kwa Nuru Njukute ambaye ni mmoja viongozi wa kitongoji kimojawapo kijiji hapo,” alieleza mtendaji huyo wa kata.
Alisema hata hivyo hawakumkuta mtendaji huyo, ndipo walipoondoka na mwenyekiti huyo hadi kwa mtendaji wa kijiji na kuingia ndani na kuwatoa nje yeye na familia yake. Alisema walivyomtoa nje na familia yake, walimchukua na kuzunguka naye nyuma ya nyumba na huko wakampiga risasi tatu na kumuua hapo hapo.
“Walivyomaliza kufanya mauaji hayo walichoma nyumba yake na wakaondoka eneo hilo na mateka wao,” alisema mtendaji huyo. Alisema mateka huyo aliwapeleka kwa kiongozi wa Kitongoji wa Londo, Michael Nicholaus ambaye alivyosikia hodi alipitia mlango mwingine akijaribu kutoroka, lakini wakampiga risasi ya kichwa ikatokea kwenye jicho.
“Hata hivyo, bahati nzuri kiongozi huyo wa kitongoji hakufariki, alijeruhiwa tu, na sasa amelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Mchukwi,” alieleza na kuongeza kuwa walipomaliza kufanya unyama huo, ndipo walimpogeukia mateka wao na wakampiga risasi na kumuua hapo hapo.
Alisema polisi walifika eneo hilo jana asubuhi wakiongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Simon Sirro. “Sirro amefika hapa na amewapa pole wananchi na amegeuza jioni hii,” alieleza mtendaji huyo.
Na Emmy Mwaipopo
Chanzo: Habarileo
Share on Google Plus

About mwanaidinuhu

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment