Tuzo za filamu ‘International Film Festival Award’ kutunisha mifuko ya wasanii


Kampuni ya Azam media kupiti Kampuni ya Azam media kupitia Channel (Idhaa) ya Sinema Zetu imeandaa Tamasha la Kimataita la Filamu hapa nchini ‘International Film Festival Award’ kwa lengo la kukuza, kuthamini kazi za Wasanii na maslahi yao pamoja na kukuza lugha adhimu ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.

Mratibu wa Tamasha hilo Bi. Zamaradi Nzowa (kulia) akizungumza na waandishi wa habari mapema leo.
Washindi hao mbalimbali wa tuzo hizo wataondoka zawadi ya tsh milioni 5, 2 na 1 pamoja na tuzo zao mkononi.
Hayo yameelezwa Jumatatu hii Jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Tamasha hilo Bi. Zamaradi Nzowa alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari juu ya uzinduzi wa Tamasha hilo ambalo litahusisha Nchi za Afrika, hususani nchi za Afrika Mashariki ambazo hutumia Lugha ya Kiswahili katika kuandaa na kuigiza filamu zao.
Bi. Nzowa alieleza kuwa Idhaa ya Sinema zetu imekuja na ujio huo mpya rasmi kwa mwaka 2017/2018 ambapo katika ujio huu ameeleza kuwa wamekuja na Tamasha la Sinema Zetu International Film Festival award, kwa lengo la kutoa tuzo kwaajili ya filamu zinazotumia lugha ya Kiswahili na pia kuweka mchango katika filamu za nchi yetu.
“Lengo kubwa la tamasha hili ni kutoa wigo mpana kwa Tasnia ya Bongo Movies (uigizaji) kwa maana ya kwamba kama channel kwa jinsi ilivyo inarusha tamthilia na sinema za Kiswahili za hapa Tanzania kwahiyo tumekaa tukaona kwamba kwa sasa tuanze kuwapa tuzo na katika safari yetu ya kuwapa tuzo pamoja na kufanya Tamasha,” alifafanua Bi.Nzowa.
Aidha aliongeza kuwa, Tamasha hilo linalotarajia kufanyika kuanzia January Mosi mwakani, litaanza katika mchakato wa kukusanya Sinema na Tamthilia kutoka kwa waigizaji wa mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar pamoja na nje ya nchi kuanzia sasa hadi tarehe 30 Novemba mwaka huu, ambapo mwezi Desemba wataanza rasmi kuchuja filamu kwaajili ya kupata filamu zitakazoingia katika kinyang’anyiro cha tuzo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Tamasha hilo Bw. Jacob Joseph alisema kuwa, wanatarajia kushirikiana na wadau wa tamasha hilo kutoka mikoani kwaajili ya kwenda kuonana na wadau wa filamu pamoja na kutoa elimu na kujenga uelewa juu ya tamasha hilo pamoja na kukusanya kazi zao.
“Hakutakuwa na upendeleo wa aina yoyote katika tamasha hili ndio maana tutakwenda mikoani kukusanya kazi za wasanii wa mikoani kwani tutakuwa hatujawatendea haki kama hatutoweza kuwafikia kwahiyo tutawafikia wakazi wa mikoani katika mikoa 11 hapa Tanzania,” alisistiza Bw. Joseph.
Aliongeza kuwa, Tamasha hilo linahusisha tuzo za aina tano ambazo ni Filamu inayoanzia saa moja na kuendelea, Tuzo za filamu fupi (Short film), Makala zenye dakika tano hadi kumi, Tuzo maalumu ya makala inayozungumzia utaifa, mshindi katika Makala maalum atapewa cheti na zawadi pamoja na tuzo ya mtu binafsi kama vile Muigizaji bora, Muongozaji bora, Mpiga picha bora Muigizaji bora wa kike na kiume n.k.
Balozi wa Tamasha hilo ambaye pia ni Muigizaji wa Bongo Movie Elizabeth Michael ‘Lulu’ ameeleza kuwa Tamasha hilo ni mkombozi wa filamu hapa nchini kwani litawafanya wasanii waamke na kutayarisha kazi zenye ubora kwa manufaa yao, kukuza kipato, pia litaongeza ushindani kwa waigizaji na kukuza Lugha adhimu ya Kiswahili.
“Pengine tupo wasanii wazuri, wapo Waongozaji wazuri, wapo wapiga picha wazuri, lakini hapakuwa na kitu cha kutupima hivyo kupitia tamasha hili tasnia yetu itaheshimika kujulikana na kusonga mbele hivyo kwetu ni jambo zuri sana” alifafanua Lulu.
Aliongeza kuwa hakuna mafanikio bila kipimo hata katika maisha mitihani ndiyo inamfanya mtu asonge mbele hivyo ujio wa Tamasha na tuzo hizi ni faraja kwani ni Tuzo zilizokuwepo hazikuwa na uwazi, usawa na wakati mwingine zilitolewa kwa kujuana, tuzo hizi zitasidia kila mmoja kufanya kazi ya uhakikia kwaajili ya ushindani kwani hazitakuwa na upendeleo wala kubebana.
Naye Prof. Martin Mhando ambaye atakuwa Msimazi wa Majaji wa tamsha hilo ameeleza kuwa hakutakuwa na upendeleo kwa mtu yeyote na kwamba ubunifu na utayarishaji bora ndiyo msingi wa tamthilia kushinda tuzo hiyo.
Tutakuwa na kituo cha kupokea Tamthilia kutoka katika mikoa, hili ni jambo jipya tumekuwa na tamasha la ZIFF kwa mikoa 10 sasa lakini tumekuwa hatupokei kazi za watu kutoka mikoani hivyo tumekuwa tukiwanyima fursa watu wa mikoani,” alisema Prof. Mhando
Tamasha la kimataifa la sinema zetu litafayika kwa mara ya kwanza hapa nchini na kilele chake kitakuwa 28 mwezi Februri 2018 ambalo litahusisha Visiwa vya Zanzibar, Miji ya Nairobi, Tanga, Arusha, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Mtwara, Morogoro, Kigali, Bujumbura, Nairobi, Kampala pamoja na Goma.
Share on Google Plus

About mwanaidinuhu

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment