Bilionea aliyetaka kununua nyumba za Lugumi ‘Dkt. Luis Shika’ kupimwa akili

Bilionea Dkt. Luis Shika ambaye wiki iliyopita alitangaza kununua nyumba za kifahari za mfanyabiashara za Said Lugumi, zilizopo eneo la Bweni JKT jijini Dar es salaam anatarajiwa kupelekwa hospitali kupimwa afya ya akili.

Hayo yamesemwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Jeshi la Polisi (SACP), Benedict Kitalika, ambapo amesema uamuzi wa kumpeleka hospitali Dkt. Shika  kuchunguzwa afya ya akili yake, umetokana na uchunguzi wa awali ulioonesha anaweza kuwa na tatizo hilo huku akidai kuwa uchunguzi huo utalisaidia Jeshi la Polisi kukamilisha uchunguzi.

“Tunatarajia kumpeleka hospitali wakati wowote ili kuangalia kama kuna tatizo katika afya ya akili au la kutokana na historia yake ya maisha inavyojionyesha, hali ambayo inaweza kutupa majibu sahihi.” amesema Kamishna Kitalika.

Kamishna Kitalika amesema uchunguzi wa awali ulihusisha historia ya maisha yake inayoonyesha ni msomi aliyewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi nchini Urusi kabla ya kurudi nchini na kuishi kwenye chumba kimoja cha kukodi, huku sababu za kurudi kwake zikiwa hazijulikani.

“Na sisi tumejiuliza sana kuhusu utimamu wa akili kama upo sawa au kuna tatizo la kisaikolojia, kwa sababu ukiangalia historia yake inaonyesha wazi ni msomi mzuri ambaye ameshika nafasi za uongozi nchini Urusi, lakini maisha anayoishi nchini si ya kuridhisha. Hatujui amepatwa na nini hadi kufikia hatua ya kukodi chumba kimoja cha kuishi katika Mtaa wa Tabata, huku mwonekano wake ukiwa haupo sawa kisaikolojia.” amesema Kamishna Kitalika.

Hata hivyo, tayari jalada la kesi ya Dkt. Shika limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili aweze kuangalia kama kuna jinai yoyote iliyotendeka kwa mtuhumiwa huyo au la.

Akizungumzia hilo, Kamishna Kitalika amesema licha ya jalada hilo kuwa mikononi mwa AG, imebainika kuwa baadhi ya kanuni wakati wa mnada wa nyumba za Lugumi hazikufuatwa, ikiwepo ya kulipa asilimia 25 pale pale baada ya mteja kujitokeza hali ambayo inaongeza shaka kwa Dkt. Shika.

“Katika mnada ule, baadhi ya kanuni hazijafuatwa ikiwamo ya kumtaka kulipa asilimia 25 pale pale mara baada ya kununua, lakini suala hilo halijafanyika badala yake waliendelea kupiga mnada nyumba nyingine, hivyo kama taasisi za uchunguzi tunapaswa kufuatilia hatua kwa hatua,” amesema Kamishna Kitalika.

Wiki iliyopita, Dkt. Shika alijitokeza kwenye mnada wa nyumba tatu za Lugumi, mbili zipo Mtaa wa Mbweni JKT na moja ipo Upanga na kushinda minada yote.

Mnada huo ulifanywa na Kampuni ya Udalali ya Yono kwa amri ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambapo Dk. Shika aliahidi kununua nyumba hizo kwa thamani ya Sh bilioni 2.3 lakini alishindwa kulipia asilimia 25 ya fedha hizo ambazo ni shilingi milioni 800 kitu ambacho kilipelekea akamatwe na polisi kwa kosa la kuharibu mnada na utapeli.

Chanzo : Mtanzania

Share on Google Plus

About mwanaidinuhu

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment