Jinsi hukumu ya Lulu itakavyokuwa mahakamani leo

Kwa ufupi

  • Lulu anakabiliwa na kesi ya kumuua mpenzi wake Steven Kanumba bila kukusudia, kinyume cha kifungu cha 195 cha kanuni za adhabu (PC), Aprili 7, 2012, Sinza Vatican jijini Dar es Salaam kufuatia ugomvi wa kimapenzi ulioibuka baina yao.
By James Magai, Mwananchi jmagai@mwananchi.co.tz
Wadau wa sanaa ya filamu nchini masikio yao leo yatakuwa katika Mahakama Kuu ambako kutakuwa na tukio kubwa katika tasnia hiyo wakati itakapotolewa hukumu ya kesi inayomkabili mwigizaji maarufu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu.
Lulu anakabiliwa na kesi ya kumuua mpenzi wake Steven Kanumba bila kukusudia, kinyume cha kifungu cha 195 cha kanuni za adhabu (PC), Aprili 7, 2012, Sinza Vatican jijini Dar es Salaam kufuatia ugomvi wa kimapenzi ulioibuka baina yao.
Hapana shaka kuwa hii ni hukumu ambayo inasubiriwa kwa hamu na wadau wa sheria, sanaa ya uigizaji, wapenzi wa filamu, ndugu, jamaa na marafiki wa mshtakiwa huyo na wa marehemu Kanumba na hata jamii kwa jumla.
Hii inatokana na ukweli kwamba ni moja ya kesi zilizovuta hisia za makundi yote katika jamii tangu kutokea kwa tukio hilo, kushtakiwa kwa msanii huyo, jinsi jamii ilivyokuwa ikifuatilia mwenendo wa kesi pamoja na kuibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya jamii na hata vijiweni.
Wakati upande wa mashtaka ukidai kuwa Lulu alimuua Kanumba bila kukusudia, Lulu mwenyewe mara zote amekuwa akikana mashtaka hayo akidai kuwa hahusiki kwa vyovyote na kifo cha mpenzi wake huyo.
Hata hivyo, mvutano huo baina ya mshtakiwa huyo na upande wa mashtaka unatarajiwa kuhitimishwa leo na Jaji Sam Rumanyika aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo.

Kama ilivyo ada kwa kesi yoyote, kila upande yaani upande wa mashtaka na wa utetezi (mshtakiwa) utakuwa unatarajiwa moja kati ya mambo mawili; mshakiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu au kuachiwa huru.
Hivyo ndivyo inavyotarajiwa kutokea pia kwa hukumu ya msanii huyo itakaposomwa na Jaji Rumanyika na kama mshtakiwa atatiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo au atabaki uraiani kuendelea na maisha kama kawaida, iwapo mahakama haitamtia hatiani.
Kwa vyovyote itakavyokuwa matokeo ya hukumu hiyo yatakuwa na uzito wa pekee kwa msanii huyo kwani ndiyo itakayotoa mustakabali wa maisha yake.
Hii ina maana kwamba iwapo apatikana na hatia, basi atakabiliwa na adhabu, jambo ambalo litabadili historia na mustakabali wa maisha yake kwa jumla, ingawa inategemeana na adhabu atakayopewa.
Lakini iwapo atashinda kesi hiyo, basi yeye ndiye atakayekuwa na furaha kubwa kwa kuwa atakuwa ameepuka adhabu, na hivyo kuendelea na maisha akiwa huru.
Kwa hiyo, wakati wa hukumu hiyo Jaji Rumanyika anatarajiwa ama kumtia hatiani na kumhukumu adhabu au kumwachia huru.
Katika kufanya hivyo, jaji huyo atazingatia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi wa pande zote, yaani upande wa mashtaka na upande wa utetezi pamoja na vielelezo mbalimbali.
Mbali na ushahidi huo na vielelezo vyake, pia Jaji Rumanyika atazingatia sheria zinazoongoza kesi za namna hiyo pamoja na uamuzi wa kesi mbalimbali zilizowahi kuamuliwa zenye mashtaka na hata mazingira yanayofafana nayo.
Katika kesi hasa za mauaji ama ya kukusudia au ya bila kukusudia huwa kuna ushahidi wa aina mbili. Mosi ni ushahidi wa moja kwa moja, yaani ushahidi wa kushuhudia tukio.
Pili, ni ushahidi wa kimazingira. Huu ni ushahidi ambao hakuna shahidi aliyeshuhudia moja kwa moja tukio likitokea, bali mshtakiwa huhusishwa na tukio kulingana na mazingira yaliyokuwapo kabla au wakati wa tukio husika.
Katika kesi ya Lulu, kwa mujibu wa Jaji Rumanyika, upande wa mashtaka umeegemea kwenye aina hii ya pili ya ushahidi wa mazingira, kwani kati ya mashahidi wanne wa upande huo hakuna hata mmoja aliyeshuhudia tukio hilo.
Ushahidi wa upande wa mashtaka unasema Kanumba alifariki dunia kutokana na tatizo la mtikisiko wa ubongo lijulikanalo kwa kitaalamu kama brain concussion, lililosababisha mfumo wa upumuaji kushindwa kufanya kazi baada ya kujibamiza ukutani upande wa kisogoni.
Hivyo upande wa mashtaka unadai kuwa mshtakiwa ndiye aliyesababisha Kanumba kujibamiza ukutani (ukimaanisha kuwa alimsukuma) na hivyo kupata tatizo lililosababisha kifo chake.
Hata hivyo, hakuna shahidi hata mmoja aliyeieleza mahakama kuwa alishudia mshtakiwa akifanya jambo ambalo lilisababisha kifo cha Kanumba, badala yake kuna ushahidi wa kusikia sauti za ugomvi baina ya Lulu na Kanumba chumbani mwa Kanumba.
Ni kutokana na sababu hiyo ndiyo maana Jaji Rumanyika wakati akitoa muhtasari wa ushahidi na kisha mwongozo kwa washauri wa mahakama kabla ya kutoa maoni yao ambao walimtia hatiani Lulu alisema kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ni ushahidi wa kimazingira.
Hivyo upande wa mashtaka unamhusisha mshtakiwa na kifo hicho kutokana na mazingira kwamba wakati Kanumba anafariki dunia, ni mshtakiwa pekee ndiye aliyekuwa naye chumbani.
Hata hivyo aina yoyote ya ushahidi, yaani wa moja kwa moja au wa kimazingira unaweza kumtia mshtakiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu kwa mujibu wa sheria, lakini ni sharti ushahidi huo uwe umethibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa pasipo kuacha shaka yoyote.
Ushahidi wa kimazingira ili uweze kumtia hatiani mshtakiwa unapaswa uwe ni ule wenye mnyororo, yaani uwe na muunganiko ambao mwisho wake humuunganisha mshtakiwa kuwa kwa vyovyote ndiye aliyefanya au aliyesababisha kifo. Hivyo ushahidi huo sharti usiwe na ‘matobo’ au usiwe umeachanaachana.
Kwa kuwa kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa ni jukumu la upande wa mashtaka, mashaka au udhaifu wowote wa ushahidi wa upande wa mashtaka unaweza kumnufaisha mshtakiwa, kwa mahakama kuamua kumwachia huru.
Kwa hiyo katika hukumu ya leo Jaji Rumanyika atachambua ushahidi wa pande zote ili kujiridhisha iwapo upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa pasipo kuacha shaka yoyote au la.
Ikiwa Jaji Rumanyika atajiridhisha kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka ama kutokana na ushahidi wake kutokuwa na uzito, kwa kutoridhisha mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kitendo ambacho kilisababisha mauti, basi atamwachia huru.
Kwa mantiki hiyo, Jaji Rumanyika atakuwa amekubaliana na utetezi wa mshtakiwa kuwa hahusiki kwa namna yoyote na kifo hicho na kuwa hakufanya jambo lolote lililosabisha kifo chake.
Hata hivyo, kama Jaji Rumanyika atajiridhisha kuwa ushahidi huo wa mazingira wa upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa pasipo kuacha shaka yoyote, basi atamtia hatiani kwa kosa hilo la kuua bila kukusudia.
Kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 198 cha kanuni za adhabu, mshtakiwa anayepatikana na hatia ya kuua bila kukusudia adhabu ya juu kabisa huwa ni kifungo cha maisha jela, ingawa imeonekana ni nadra kutolewa kwa adhabu hiyo.
Adhabu ya chini huwa ni kuachiwa huru kwa masharti maalumu au kifungo cha nje, ambapo ama mshtakiwa huonywa asifanye kosa jingine ndani ya muda maalumu unaopangwa na mahakama au anaweza kuamuriwa kufanya shughuli za jamii. Hii maana yake ni kwamba kifungu hicho kinampa mamlaka au uhuru Jaji kukadiria adhabu kwa kadri anavyoona inafaa na hasa kwa kuzingatia mambo mengine yamhusuyo mshtakiwa ama kesi kwa ujumla wake hususan mazingira ya tukio.
Jambo jingine ambalo jaji anaweza kulizingatia katika kutoa adhabu ni muda ambao mshtakiwa anakuwa ameutumia akiwa mahabusu, kwa wale ambao wanabakia mahabusu kwa sababu mbalimbali, ingawa shtaka la Lulu lina dhamana.
Kwa msingi huo baada ya kumtia hatiani mshtakiwa, Jaji anaweza kumhukumu adhabu ya miaka 20 au zaidi ama chini ya hiyo kama vile miaka 10, mitano na wakati mwingine hata miezi, na hata siku au chini ya hapo.
Ipo kesi moja ambayo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliwahi kumhukumu mshtakiwa adhabu ya kifungo cha muda wa kuanzia wakati Jaji alipokuwa akitoa adhabu hadi mahakama ilipoisha.
Yaani baada ya jaji kumaliza tu kutoa adhabu hiyo na kunyanyuka kwenye kiti chake akitoka mahakamani hapo kurejea ofisini na adhabu ya mshtakiwa nayo ikawa imeisha.
Kwa maana hiyo mtiwa hatiani huyo alitumikia adhabu ya kifungo jela kwa muda wa dakika ambazo jaji alikuwa akisoma hukumu, adhabu ambayo hata hivyo alimaliza kutumikia bado angali mahakamani kabla ya kupelekwa jela.
Hivyo hata katika hukumu ya Lulu pia inatarajiwa kuwa katika sura kama hizo, yaani mojawapo kati ya mambo hayo ndiyo yanayotarajiwa kutokea.

Kesho mbali na hukumu kamili ya msanii huyo pia tutakuletea mtiririko wa matukio muhimu katika kesi hiyo mwanzo hadi mwisho, tangu ugomvi ulivyoanza, mtuhumiwa kukamatwa, kushtakiwa kuachiwa kwa dhamana mwenendo mzima wa kesi mpaka hukumu ya mahakama.
Makala ;;Mwananchi
Share on Google Plus

About mwanaidinuhu

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment