Mjasiriamali Carol Ndosi amuandikia barua ya wazi Rais Magufuli

Mjasiriamali maarufu nchini Tanzania, Carol Ndosi amemuandikia barua ya wazi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akifikisha kilio chake kwa kugusia mambo makubwa matatu.

Jambo la Kwanza, Bi. Ndosi amemuomba Rais Magufuli aangalie upya kuhusu suala la wanafunzi wa kike wanaopata mimba kutorudi mashuleni, kwani agizo hilo alilotoa mwaka jana litapelekea watoto wa kike 8,000 kila mwaka kuacha shule.
Carol Ndosi

Mambo mengine aliyoyazungumzia ni kuhusu hali ya usalama kwa wananchi na muktadha wa demokrasia nchini kuhusu matukio yanayoendelea nchini likiwemo la kupigwa risasi kwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilini Akwelina. Soma barua hiyo kwa undani
BARUA YA WAZI KWA MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI
Mheshimiwa Rais wangu mpendwa Dr John Joseph Pombe Magufuli, Shikamoo. Natumai ni mzima wa afya na unaendelea kutimizia wajibu wa kazi ya taasisi yako. Nimeona ulikua kwenye kikao cha wakuu wa nchi za Afrika Mashariki nchini Uganda. Pole na Safari.
Kati ya mambo niliyofarijika kuyasikia ni pale wewe na Mhe. Uhuru Kenyatta mlipowaambia mawaziri wa wizara husika wakae chini ma kushughulikia migorogoro midogo iliyokua inajitokeza hivi karibuni na kuharibu mahusiana ya nchi zetu mbili. Hakika sisi ni jumuiya na yatupasa kufanya kila namna kulinda jumuiya hii.
Mhe. Rais wangu mpendwa Dr John Pombe Magufuli, nimeona pia ulivyorudi, umepitia Mwanza kwanza. Mwanza ni mikoa ambayo naipenda sana pia kutokana na mazingira ya kibiashara yaliyopo na hata wakazi wa huko walivyo wakarimu. Kupitia matamasha yetu ya na shughuli za The Launch Pad za uwezeshaji wa vijana na wanawake, tunatarajia kuendelea kushirikiana na wananchi wa mkoa huu kuendelea kutengeneza ajira, kutangaza mkoa na kuwawezesha vijana na ujuzi wa ujasiriamali na kutafuta ajira.
Hakika ni wakazi wenye kujituma sana kwenye nyanja mbalimbali. Hawatofautiani sana na wakazi wa Kimara, waliokua na nyumba zao, maisha na biashara kwenye maeneo waliyobomolewa kwa agizo na mpango wa serikali. Nawaza tu, tamko lako kwa wakazi wa Mwanza waliokua wabomolewe makazi yao limenipa faraja sana. Hata hivyo limenipa pia simanzi na kuwaza je kama wenzetu wa Kimara wangepata kusikia kutoka kwako rais wetu mpendwa kabla hawajapoteza mali na mustakabali wa maisha yao, hakika leo hii tusingekua tunasikia vilio na laana kutoka kwa waathirika wa ubomoaji Kimara.
Rais wangu mpendwa Dr John Pombe Magufuli, nakumbuka kukufuatilia sana uchapaji wako wa kazi ulivyokua waziri, tena tumeshakutana kwenye press conference na mikutano mbali mbali nilivyokua mwandishi wa habari ninayeingia field. Ulikua unanipa faraja sana kuona kuna viongozi ambao ‘they walk the talk’. Actually kipindi kile ilikua no talk sana kwako mengi yalikua ni vitendo. Ni historia yako hii iliyonipa faraja hata matokeo yalivyo tangazwa kuwa umeshinda uchaguzi wa urais (niseme ukweli nilimpigia kura Mama Anna Mghwira, I am an unapologetic feminist fortunately).
Ni mmoja kati ya wale walioamini kabisa katika nia na dira yako uliyoingia nayo ya kwanza kuwa mtetezi wa wanyonge, yaani nilikua nina imani sana kuwa wale wanyonge ambao kwa mtazamo wangu ndio majority ya Watanzania, ungeweza kuwafikia kwa huduma zote za msingi za kijamii. Niliamini kabisa kwa nia yako ya kuanza safari ya Tanzania ya viwanda, itatukomboa kiuchumi na kimaendeleo.
Ulipoanza na kupunguza matumizi ya Serikali na safari zisizo na tija kwa maendeleo ya nchi, mimi na wenzangu wengi tulifarijika sana. Makinikia ndio ilikua iwe homerun, bado tuna imani, Hakika hata msemo wako wa ‘Hapa Kazi Tu’ ulinipa muamsho mpya wa kujituma zaidi, binafsi hata na changamoto zote nilizokua napitia, zingine zinazohusiana na maamuzi ya viongozi wengine serikali kwa wafanyabiashara kama sisi, nilijitahidi kutokata tamaa na kuendelea na KAZI hadi pale nilipo komolewa kuliko. Mimi ni yule niliyeandika barua kwako mjasiriamali ambayo ilieleza changamoto tulizo pitia kama mtayarishaji wa tamasha na jinsi tulivyo athirika na kufungiwa kwa Uwanja wa Leaders na sheria mpya ya matamasha ambayo hata hivyo imeonekana kubagua.
Rais wangu mpendwa Dr John Pombe Magufuli, bado nina imani una nia njema kabisa na Watanzania. Naamini hili kupitia jitihada zako mbali mbali za miradi ya maendeleo haswa ya miundo mbinu. Wengi wanahoji ‘priorities’ na kama zina-akisi ‘utetezi wa wanyonge’. Hawajaona SGR na Flyover zinawasaidia vipi wanyonge kwa sasa. Huwa najibu inawezekana kabisa hatujui ‘grand vision’ yako kwa ajili ya Tanzania. Tukupe muda kidogo.
Kama Mtanzania niliyejaliwa vipaji na ujuzi katika nyanja mbali mbali, Nilichoka kulalamika, kila ninachofanya actually najaribu kuendana na mpango wa maendeleo wa taifa #FYDP, jinsi gani ninaweza kusupport jitihada za serikali kwa nafasi na platform zangu.
Na kwa heshima zote na taadhima Ndio maana ulivyo tuhakikishia mtoto wa kike mwenye kupata mimba kutoruhusiwa kurudi shuleni, na ulivyo sisitiza kuwa unajitahidi kuweka elimu bure halafu watoto wa kike wanachezea nafasi kwa kupata mimba, hadi ukasema ‘mkitaka wajengeeni shule au waende VETA’, niliyabeba haya na kusema kweli ingawa ni haki ya mtoto kupata shule, lakini Rais wetu hili hebu ngoja tutafute suluhishi hadi pale ambapo ungekaa na kutufikiria tena baba.
Nasema kutufikiria tena sababu naamini kabisa kama mtetezi wa wanyonge, hutokubali kuwaacha wasichana zaidi ya 8000 wanaoacha shule kila mwaka kutokana na mimba za utotoni. Hakika hawa ni nguvu kazi ambao tunawahitaji kusukuma gurudumu la maendeleo na hata Tanzania ya viwanda.
Nilikaa na kufikiria jinsi gani ya kukuunga mkono kwenye hili, mimi ndio yule uliyeambiwa ninaye shirikiana na watanzania kujenga shule ya waathirika wa mimba na ndoa za utotoni. Shule hii itakua ya Ujuzi na Stadi Za Kazi ili kuunga jitihada za Tanzania ya Viwanda na dhana ya kuongeza thamani kwenye uzalishaji.
Rais wangu mpendwa Dr John Pombe Magufuli, umesikia matukio ambayo kwa kweli YANATISHA mno na kubadilisha historia nzima ya nchi yetu kama jamii inayoheshimu sheria na kuendeleza amani. Naamini kabisa huyafurahii haya.
Kutoka waathirika wa matukio ya Zanzibar, hadi maaskari wa Kibiti, na sasa haya kisiasa yanayo ripotiwa kila siku. Kwa jinsi ninavyo amini ulivyo muumini wa Mungu na hata kututamkia ni Mungu ndiye anaye kuongoza, lazima itakua inakusikitisha na kukuuma mno kuona wananchi wako wanavamiwa kwa mashambulizi ya risasi, wengine hadi kupigwa risasi 30 NA! Na hata kijana mdogo kama Akwilina Akwilin Bafta kupoteza maisha kwa risasi.
Nawaza sana wakati mgumu unaopitia sasa maana naona kabisa nia uliyo kuwa nayo na sisi kama taifa inazidi kuchafuliwa. Najiuliza mimi kama Mtanzania ninaye jitahidi kufanya kila niwezalo kuchangia maendeleo ya nchi yangu na kutetea katiba na haki za wananchi nikusaidie vipi ili uweze kuendeleza nia yako.
Nikuombe pia uongee na sisi baba. Wewe ni baba yetu, tunahitaji kusikia kutoka kwako nchi inaelekea wapi na haya matukio na uminywaji wa demokrasia na kutumika vibaya kwa mamlaka kwa baadhi ya viongozi na taasisi. Naomba nikuhakikishie hamna Mtanzania anayefurahia haya yanayoendelea na wala hamna ambaye anakinzana na nia yako njema ya kuleta maendeleo na usawa katika taifa hili. Tuko na wewe, kila Mtanzania kwa nafasi, uwezo na uwepo wake.
Wengi wangependa kuwepo na mazingira yatakayo wawezesha wao kutimiza wajibu na nafasi zao kama Watanzania kuleta maendeleo nchini na kwenye maisha na jamii zao. Kila kukicha naona manung’uniko ya Watanzania kuhusu mambo mbali mbali. Nakataa kuendelea kuwa jamii inayolalama kila siku haswa kwa haya tunayo yalalamikia. It has to end.
Tunaomba na Tunakuhitaji sana utumie mamlaka yako uliyopewa na Mamilioni ya Watanzania kuhakikisha matukio haya, uminywaji wa haki za binadamu, ukiukwaji wa katiba na demokrasia, na matumizi mabaya ya viongozi na mamlaka YANAFIKA KIKOMO.
Rais wangu mpendwa Dr John Pombe Magufuli, Sijui utaona suluhishi gani linafaa kuondokana na hii hali ya sasa hivi, Katiba mpya ingekua ni kipaumbele hakika mengi yasingetokea. Sijui pia kama kuna nafasi ya kukaa chini na ya kuyajadili haya kama taifa. We are not happy baba. We are hurting. From our very cores.
Wako MNYENYEKEVU katika Ujenzi wa Taifa
Carol Ndosi
Share on Google Plus

About mwanaidinuhu

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment