Madai Yaibuka Je Agness Gerald aka Masogange Ameuawa???

WAKATI mwili wa ‘Video Queen’ maarufu Bongo, Agness Gerald ‘Masogange’ ukitarajiwa kuzikwa jana nyumbani kwao Utengula, Mbalizi-Mbeya, utata umeibuka juu ya kifo hicho kufuatia kuibuka kwa madai kuwa mrembo huyo ameuawa.

Masogange alipatwa na umauti huo, Ijumaa iliyopita katika Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge jijini Dar alipokuwa amelazwa kwa takriban siku nne ambapo taarifa za awali zilieleza kuwa, mrembo huyo amefariki kwa ugonjwa Pneunomia (nimonia) na tatizo la kupungua damu.


 MADAI YA KUUAWA YAIBUKA

Mara baada ya kifo hicho kutokea, taarifa mbalimbali zilibuka na kutawala kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa Masogange ameuawa kutokana na kifo hicho kuwa cha ghafla.

“Inabidi kwa kweli uchunguzi wa kina ufanyike. Kifo chake kimekuwa cha ghafla mno, hajaumwa kiivyo na watu wengi tulikuwa tunajua ni mzima wa afya,” waliandika watu tofauti mitandaoni.

 WENGINE WAHUSISHA NA SIASA

Wengine walienda mbali zaidi kwa kukihusisha kifo hicho na masuala ya kisiasa huku wengine wakihusisha kifo chake na vigogo wa madawa ya kulevya.

Uwazi lilizungumza na majirani mbalimbali waliokuwa wanaishi na Masogange, maeneo ya Makongo Juu jijini Dar ambao walionesha kushtushwa na taarifa hizo za kuuawa huku wengi wakiliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi ili kuondoa huo utata.

“Kwa kweli tumeshtuka sana maana haya madai yalianza taratibu lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda ndipo yanavyoongezeka nguvu, sasa ni vizuri polisi wakajiridhisha,” alisema Abdul, mkazi wa Makongo Juu.

POLISI WAINGILIA KATI Wakati mamia ya waombolezaji wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya kuuaga mwili wa Masogange juzi Jumapili katika Viwanja vya Leaders Kinondoni jijini Dar es Salaam, polisi walilazimika kufika kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kujiridhisha kutokana na madai hayo ya kuuawa.

 Wanahabari wetu waliofuatilia hatua kwa hatua kifo hadi mazishi ya video queen huyo, walishuhudia polisi wakizuia kwa muda mwili huo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hali ambayo ilisababisha ratiba za ibada ya kuaga mwili huo kuchelewa kuanza. Awali, ratiba ilionesha kuwa mwili huo ungechukuliwa Muhimbili mishale ya saa 2 asubuhi ili ratiba ya kuagwa ianze saa 3 kamili lakini kutokana na uchunguzi huo wa polisi, ratiba ya kumuaga mrembo huyo ilianza saa 6 kamili viwanjani hapo.

SOMA PIA: Job Opportunities at Tanzania Posts Corporation, Regional Managers

MIKE SANGU ANENA

Uwazi lilizungumza na mmoja wa waigizaji ambao walienda kuuchukua mwili huo, Mike Sangu ambaye aliweka wazi kuwa walilazimika kuchelewa kuanza kwa ratiba ya kumuaga kama walivyokuwa wamepanga awali. “Tulipanga hapa tuwe tumeondoka kabla ya saa 3 ili pale Leaders ratiba ianze saa 3 kamili lakini ndio hivyo tena polisi wamesema hadi wakamilishe kwanza uchunguzi wao ndio tukabidhiwe mwili,” alisema Mike.

MSEMAJI WA MUHIMBILI AFUNGUKA

Uwazi lilizungumza na Msemaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha ambaye alithibitisha polisi kufika hospitalini hapo na kuuchunguza mwili huo kwa ajili ya kujiridhisha kabla ya kuuruhusu mwili huo kwenda kuzikwa.

“Ni kweli, walifika kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi ili kujiridhisha sababu za kifo kama unavyojua ni kifo cha ghafla,” alisema Aminiel. Hata hivyo, baadhi ya watu waliofika msibani walionesha wasiwasi wao baada ya kujua kuwa polisi waliamua kuufanyia uchunguzi mwili wa msanii huyo na kujiuliza kulikoni?

POLISI WANASEMAJE?

Uwazi lilitafuta Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ACP Salum Hamduni na ili kujua kama ana taarifa za uchunguzi huo uliofanywa na polisi lakini hata hivyo alisema hana taarifa za uchunguzi huo.

Uwazi halikuishia hapo, lilifanya jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Murilo Jumanne Murilo lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda kufuatia simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa baada ya kupigiwa mara nyingi. Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,(ZPC) Lazaro Mambosasa alipotafutwa na gazeti hili, alisema yupo mkoani Mbeya, hivyo hana taarifa rasmi kuhusu suala hilo.


TUJIKUMBUSHE

Kabla ya kukutwa na umauti huo, Masogane aliyeuza sura kwenye video mbalimbali za wasani wa Bongo Fleva ikiwemo Magubegube (Barnaba Elias), Msambinungwa (Tunda Man), aliwahi kupata misukosuko ya kuhusishwa na madawa ya kulevya.

Mwaka 2013, Masogange alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Oriver Tambo nchini Afrika Kusini akidaiwa kusafirisha madawa ya kulevya aina ya Crystal Methamhetamine.Hata hivyo, baada ya kesi kuunguruma nchini humo, ilibainika kuwa hayakuwa madawa ya kulevya bali ni malighafi za kutengenezea madawa hivyo Masongange aliachiwa baada ya kulipa faini.

 Mwaka jana, Masogange alitajwa na kuunganishwa kwenye kesi ya matumizi ya madawa ya kulevya baada ya kutajwa katika orodha ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipokuwa akiendesha oparesheni ya watumiaji na wauzaji wa madawa ya kulevya.

Kesi iliunguruma hadi Aprili 3, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar ilipotolewa hukumu kwa mrembo huyo kutakiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya shilingi milioni moja na nusu.Masogange alilipa faini hiyo na hivyo kuwa huru hadi alipopatwa na umauti Ijumaa iliyopita.

Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, amina!

STORI: GPL 
Share on Google Plus

About mwanaidinuhu

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments/maoni:

Post a Comment